TRA yatangaza msamaha wa riba na adhabu za kodi

Mtanzania - - Mbele - Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imetangaza kutoa msamaha, riba na adhabu hadi asilimia 100 kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi tofauti na asilimia 50 ya awali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere jana, lengo la msamaha huo ni kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu kwa kulipa malimbikizo ya madeni ya msingi kwa awamu ndani ya mwaka 2018/19.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa msamaha wa riba na adhabu utahusu kodi zote zinazotozwa kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na TRA.

“Msamaha huo unahusu ushuru wa forodha unaosimamiwa chini ya Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004, mapato mengine yasiyo ya kodi ambayo TRA imepewa jukumu la sheria kuyakusanya.

“Mapato hayo ni kama vile kodi za majengo na ada za matangazo.

“Walipakodi watakaonufaika na utaratibu huu watatakiwa kuwa na sifa zifuatazo; kwanza wawe wamewasilisha ritani za kodi lakini bado wanadaiwa kodi yote au sehemu ya kodi zitokanazo na ritani hizo.

“Hawajawasilisha ritani za kodi na wana madeni ya kodi, ambao walikuwa wanafanya biashara bila kusajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), namba ya usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VRN) au usajili mwingine wa kodi kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na TRA.

“Waliowasilisha pingamizi za kodi kwa Kamishna Mkuu na ambao pingamizi zao bado zinashughulikiwa katika ofisi za TRA na si kwenye mahakama za ikodi.

“Ambao wamewasilisha pingamizi katika mahakama za kodi na mashauri yao bado hayajatolewa uamuzi, ambao wana madeni ya nyuma ya kodi ambayo hayatokani na kesi za jinai za kodi, utakatishaji fedha, usafirishaji wa binadamu au shughuli nyingine haramu,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema mlipakodi atastahili kupata msamaha wa riba na adhabu endapo yeye binafsi au mwakilishi wake aliyeidhinishwa katika sheria atawasilisha maombi ya msamaha kwa kujaza fomu maalumu Na.ITX207.01.E.

“Fomu hiyo inapatikana katika tovuti ya TRA ikiambatana na maelezo ya kuonyesha kiasi anachodaiwa pamoja na kukubali kwa hiari kulipa deni lake la msingi “Principal Tax”.

“Kukubali kwa maandishi kulipa kiasi chote cha kodi bila riba na adhabu ndani ya mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa na maana kabla au ifikapo Juni 30 mwaka 2019.

“Kwa madeni yaliyo katika pingamizi; kukubali deni la kodi alilokadiriwa na kuwa tayari kutoendelea na pingamizi au shauri husika la kodi lililowasilishwa kwa Kamishna Mkuu, Bodi ya Rufani za Kodi au Mahakama ya Rufaa.

“Hata hivyo, msamaha utatolewa kwa maombi yatakayokidhi masharti na kukubaliwa na TRA ambako Kamishna Mkuu wa TRA na mlipakodi husika watasaini mkataba wa makubaliano utakaoanisha deni lote la kodi; riba na adhabu inayosamehewa, pamoja na kodi isiyo na riba wala adhabu itakayopaswa kulipwa kabla ya Juni 30 mwaka 2019.

“TRA inawahimiza walipakodi wote nchini kuitumia fursa hii adhimu kwa kushiriki kwa ukamilifu katika hatua hii maalumu ya utoaji wa msamaha wa riba na adhabu.

“Utoaji wa taarifa sizizo sahihi ni kosa katika sheria, endapo itabainika hivyo itasababisha mwombaji kupoteza sifa ya kufaidika na msamaha huu,”ilisema taarifa hiyo.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.