Wazazi wenye watoto walemavu hoi kwa uchumi

Mtanzania - - Habari - Na LILIAN JUSTICE

WAZAZI wa watoto wenye ulemavu wa akili na viungo wametajwa kukabiliwa na changamoto za uchumi kwa kutumia muda mwingi kuhudumia watoto wao bila kufanya shughuli za kujiongezea kipato.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa akili na viungo cha EMFERD, Josephine Bakhita kwenye semina ya uhamasishaji na maelekezo ya namna ya kuwapa huduma bora watoto wenye ulemavu wa akili na viungo.

Alisema wazazi wa watoto wenye ulemavu wa aina hiyo wanatumia muda mwingi kuwalea watoto hao badala ya kwenda shambani kulima au kufanya biashara nyingine za kujiletea kipato. Mkurugenzi huyo aliwasihi wazazi au walezi wenye watoto walemavu kuendelea kuwapa huduma watoto wao bila kukata tama wala kujisikia vibaya.

“Kamwe msikatishwe tamaa kwa kuwa mna watoto wenye ulemavu wa akili na viungo.

“Binafsi nilikuwa na mtoto mwenye ulemavu wa aina hiyo hiyo na niliweza kumlea kwa upendo mpaka alipofikia umri wa utu uzima,’’alisema Bakhita.

Hata hivyo, Bhakita alitoa wito kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa akili na viungo kujifunza kazi za mikono na kufanya shughuli za uzalishaji mali maeneo ya karibu na nyumbani ili kuendelea kuwa karibu na watoto wao.

Mmoja wa wazazi wenye watoto walemavu, Mwajuma Ibrahimu kutoka Kijiji cha Makuyu wilayani Mvomero, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni kwamba mtoto mwenye ulemavu wa akili hawezi kuachwa nyumbani peke yake wala kumwachia jirani.

‘’Muda wote mtoto huyu anahitaji uangalizi wa pekee wa mzazi hivyo inakuwa vigumu mzazi kupata nafasi ya kufanya shughuli nyingine za maedeleo kama wengine,” alisema Ibrahimu.

Awali, Ofisa Tarafa ya Wilaya ya Mvomero, Winfred Kipako aliwasisitiza wazazi kuacha kuwapeleka watoto wenye matatizo kwa waganga wa jadi kwa sababu ulemavu mwingine unasababishwa na ucheleweshaji wa tiba na tiba zisizo za uhakika.

Tengenezeni viatu imara ambavyo mtu akivaa hajutii kwa sababu ya ubora wake - Charles Mwijage Bendera zinazopepea katika magari ya mawaziri, nyingi zimechanika na kubaki nyuzi - Dk. Philip Mpango

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.