Takukuru kuchunguza kampuni Simba Trust

Mtanzania - - Matangazo/habari - Na MWANDISHI WETU

SIKU moja baada ya kuibuka kwa mjadala wa walipo wamiliki wa Kampuni ya Simba Trust, hatimaye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imevunja ukimya na kusema bado wanaendelea na uchunguzi wa sakata hilo.

Akizungumza jana Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishana Valentino Mlowola, alisema kuwa kwa sasa taasisi yake inaendelea na uchunguzi wa suala hilo ingawa tayari baadhi ya wahusika akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya PAP/ IPTL, Habinder Singh Sethi na mwenzake wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira tayari wapo mahakamani.

Kamishana Mlowola, alisema kuwa kwa mujibu wa utaratibu Takukuru inapokuwa kwenye uchunguzi wa suala lolote ikiwamo kama la Simba Trust, halipaswi kuzungumzwa hadharani kwani kuna maeneo yanatahusika kwenye ushahidi pindi kesi ya msingi inatakapoanza kusikilizwa na mahakama.

“Kwa sasa siwezi kusema lolote kwa sasa ingawa ninachojua ninachojua kwa sasa tuna kesi mahakamani na kina Sethi mahakamani. Kwa hiyo yapo mambo tunaweza kusema kwamba kuyazungumza kwa sasa tutakuwa tunaingilia masuala ya uchunguzi ambao tunaendelea nao,” alisema Kamishna Mlowola

Hata hivyo kwa sasa wakati serikali ikiendelea kumshikilia aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya PAP/ IPTL, Habinder Singh Sethi, wamiliki wenza wa kampuni ya Simba Trust hawajulikani walipo huku kigogo huyo akiendelea kusota mahabusu.

Sethi pamoja na aliyekuwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, wako mahabusu kwa sasa wakibiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 300.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Kampuni ya Simba Trust ambayo ilinunua hisa asilimia 50 kwenye kampuni ya PAP iliyonunua hisa zote za IPTL iliyoliingiza taifa kwenye hasara, sasa inadaiwa kumtekeleza mbia wake Sethi.

Simba Trust imesajiliwa Australia kwa uwakilishi wa mwanasheria mmoja wa nchi hiyo mwenye ukaribu na baadhi ya waliowahi kuwa viongozi wa serikali katika awamu zilizopita.

Hapa nchini kampuni hiyo inatajwa kunufaika na uchotwaji wa mabilioni ya fedha ya Escrow huku taarifa ya iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), katika Bunge la 10 lililoongozwa na Spika mstaafu, Anne Makinda, iliihoji serikali kuhusu uhalali wa kampuni hiyo na wamiliki wake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.