Waziri akerwa bendera kuchanika magari ya viongozi

Mtanzania - - Habari Za Sabasaba -

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Philip Mpango, alisema anakerwa na kitendo cha bendera katika magari ya viongozi na wengine wa Serikali kuchanika na kubaki nyuzi hivyo kuwataka wakala wa huduma ya ununuzi serikalini (GPSA) kuhakikisha wanabadili bendera hizo vinginevyo hatua kali zitachukuliwa.

Mpango alisema hayo alipotembelea banda la wizara ya fedha lililo na taasisi zilizo chini yake katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa ya Sabasaba na kusisitiza kuwa alishawapigia simu kuhusu ubora wa bendera hizo lakini bado hazijabadilishwa.

“Sitaki kuona hali hiyo tena vinginevyo nitachukua hatua kwani nilishawapigia simu kuwaeleza ubora wa bendera zinazopepea katika magari ya mawaziri, nyingi zimechanika ikiwemo yangu na kubaki nyuzi tu,” alisema Mpango.

Alisema bendera ni alama ya taifa inahitaji heshima na Watanzania wanahitaji kuona alama hizo zikiwa na ubora, ni vema kuangalia zote zilizopo barabarani kuhakikisha hakuna inayopepea ikiwa imechanika kwani unakuta waziri akinunua bendera na kutembea kutoka Kibaha mpaka Chanika inakuwa imeishachanika.

Awali alipotembelea banda la Bodi ya Wataalamu wa Masuala ya Manunuzi na Ugavi (PSPTB), alisema sheria ya kuwabana wataalamu wa masuala ya ununuzi na usambazaji vifaa bado si kali kama anavyotaka ni vema waharibifu kutangazwa kwa umma.

Alisema wananchi wanavuja jasho kwa ajili ya kulipa kodi wakiwamo wengine wanatia huruma katika kulipa kodi huku wachache wakizila fedha hizo ndani ya Serikali, hivyo ni vema bodi hiyo kusimamia kwa nguvu wataalamu wao serikalini ili kuzuia upotevu wa fedha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.