Aibu gari la Serikali kusafirisha mirungi

Mtanzania - - Tahariri -

KATIKA toleo la leo la gazeti hili, tumechapisha habari kuhusu kukamatwa kwa gari la kubebea wagonjwa la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, likituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.

Kukamatwa kwa gari hili kulitokana na mtego uliokuwa umewekwa na polisi wilayani Bunda, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba DFPA 2955, lilikamatwa likiwa na magunia 34 ya mirungi yenye uzito wa kilo 821, yakisafirishwa kwenda mkoani Mwanza.

Tukio hili lilitokea Julai 10, mwaka huu saa 10 alasiri katika Kijiji cha Bitaraguru wilayani Bunda, huku likiendeshwa na George Matai, ambaye ni mwajiriwa wa halmashauri akiwa na mkazi wa Sirari, Ruda Joseph wakitoka Kijiji cha Nyanchabakenye.

Tunaamini kazi nzuri iliyofanywa na polisi katika ukamataji huu, itakamilishwa kwa uchunguzi wa kina ili sheria ichukuwe mkondo wake.

Inasikitisha kuona gari la umma la kubeba wagonjwa, linageuzwa kuwa la kusafirishia mirungi, tukitambua wazi kwamba sheria za nchi hii zinakataza biashara hiyo.

Mirungi imekuwa na athari kubwa kwa jamii, hasa kwa vijana ambao wamekuwa wakiathirika baada ya kutumia na kupoteza nguvu kazi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Jambo hili linapaswa kuchunguzwa kwa kina zaidi, inawezekana mtumishi huyo wa Serikali na mtu aliyekamatwa naye hawakuanza biashara hiyo jana wala juzi, kwa sababu hadi kufikia mtu kutumia gari la wagonjwa namna hii, inaonyesha kuna ukomavu mkubwa. Tukio hili limeteleta taswira mbaya na isiyokubalika kuona gari za Serikali linashiriki vitendo haramu kama hivi.

Hapa ndiyo tunapaswa kujiuliza maswali ya msingi. Je, huyo dereva ana sifa zinazotakiwa hadi akaajiriwa ndani ya mfumo wa Serikali? Na kama hakuna nani aliyemsaidia kupata nafasi hiyo.

Tunakubaliana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, kwamba tukio hili limezidi kuuchafua mkoa huo na kuendelea kuonekana ni wenye matukio ya ajabu kila kukicha.

Tunatambua namna ambavyo Serikali imekuwa ikihaha kutafuta magari ya kusaidia wagonjwa, sasa inakuwaje watumishi wasio waaminifu wanayatumia kufanya kazi ambazo hazihitajiki?

Ndiyo maana tunasema katika hili lazima polisi wafanye kazi ya ziada katika upelelezi kwa sababu, tunaamini kuna mtandao mkubwa ndani na nje ya mkoa huo.

Wapo mamia ya wananchi hasa maeneo ya vijijini wanaotaabika kwa kukosa huduma, wakati mtumishi mmoja asiyekuwa mwaminifu anatenda upuuzi kama huu.

Kwa mfano dereva huyo, alipoteza muda mwingi wa kusimama eneo hilo na kupakia mizigo, tukiamini wapo wajawazito au wagonjwa wa dharura waliokuwa wanahitaji usafiri huo ili kuokoa maisha yao, yeye hilo hakulifikiria.

Inasikitisha kuona mtumishi huyo anatanguliza masilahi binafsi kwa kutumia gari la Serikali tena kibaya zaidi kushiriki biashara haramu.

Sisi MTANZANIA, kwanza tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa kukamata gari hilo na kulishauri kuongeza umakini kwa kila gari liwe na mtu binafsi au Serikali maana njia za uhalifu zimeongezeka maradufu.

Lakini tunatoa rai kwa jeshi hilo, kufanya uchunguzi haraka na kuachia gari ambalo wanalishikilia kama kidhibiti ili lilirudi Tarime kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wenye uhitaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.