Utafiti wa Twaweza mfupa mgumu

Mtanzania - - Mbele - Na ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM

SAKATA la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kuiandikia barua taasisi ya Twaweza kuitaka ijieleze ni kwanini isichukuliwe hatua kwa kukiuka sehemu ya 11 ya Mwongozo wa Taifa wa Usajili na Utoaji wa Matokeo ya Tafiti, limeonekana kuwa mfupa mgumu baada ya tume hiyo kushindwa kujibu maswali ya waandishi wa habari.

Wakati Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Dk. Amos Nungu, jana akilalamikia kitendo cha barua hiyo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wao Twaweza wamekana kushiriki kuisambaza.

Barua ya Costech kwenda Twaweza, iliandikwa Julai 9 na kusainiwa na Dk. Nungu, ikisema Twaweza ilikiuka kifungu hicho kupitia utafiti wake wa ‘Sauti za Wananchi’, ambao matokeo yake yalitolewa Julai 5, mwaka huu.

Matokeo ya utafiti huo, yalionyesha umaarufu wa rais, wabunge, madiwani, wenyeviti wa mitaa, vijiji na vyama vya siasa umeshuka.

Jana, Dk Nungu, alisema tume yao imesikitishwa kwa kitendo cha barua hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, huku Twaweza nao wakikana kuisambaza. Alisema katika kutekeleza majukumu yao, tume hiyo imekuwa na kawaida ya kuwasiliana na wadau pale wanapobaini utafiti unafanyika bila kusajiliwa au kufuata taratibu.

“Mawasiliano na wadau wetu ni pamoja na kuandika barua kwa taasisi au mtafiti husika. Sasa baada ya kufuatilia barua inayosambaa katika mitandao ya kijamii, tumejiridhisha kuwa ni barua halali iliyopelekwa katika Taasisi ya Twaweza ili kupata ufafanuzi wa tafiti yao.

“Tunasikitika kuona mawasiliano halali ya kiofisi yanapelekwa mitandaoni hata kabla ya kujibiwa rasmi,” alisema Dk. Nungu.

Alisema barua hiyo si ya kwanza na wamekuwa wakiandika kwenda kwa wadau mara kadhaa.

Pamoja na mambo mengine, waandishi wa habari walimwuliza Dk. Nungu kuhusu tume yake kuiandikia barua Twaweza wakati huu ambao utafiti wao umeonyesha umaarufu wa Rais John Magufuli kushuka, lakini katika tafiti zilizopita ambazo zilionyesha umaarufu wa kiongozi huyo kuwa juu, hawakuwahi kufanya hivyo. Akijibu swali hilo, Dk. Nungu alisema; “Si mara ya kwanza kuandika barua hizo na Twaweza si wa kwanza kuandikiwa barua za aina hiyo, lakini zilikuwa haziji kwenye mitandao ya kijamii.

“Sisi tunaangalia taratibu zikoje za kusajili tafiti hapa nchini, sasa hilo nadhani tukianza kuongelea hiyo barua wakati wao hawajaijibu si sahihi. Tuwape nafasi wao kujibu,” alisema.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Costech, Zainab Bakari, alishindwa kufafanua vifungu vya sheria walivyotumia akisema mkutano huo hauhusiani na barua ya Twaweza.

“Sidhani kama mkutano huu ni kwa ajili ya Twaweza, bali ni kwa ajili ya kufafanua taratibu ambazo Costech inafanya kwa ajili ya vibali vya tafiti, lakini hatuko hapa kuongelea barua za Twaweza.

“Tuna ‘guideline’ (miongozo) ambazo zimekuwa zikitumika na hiyo kamati ambayo inapitia michakato yote na hatimaye inatoa tafiti, taratibu zimekuwepo siku zote na hatimaye mwaka huu zimekuwa ‘reviewed’.

“Sheria ‘ina-provide’ hivyo na imeanzisha hiyo kamati na ni kamati ya bodi na kuna ‘guidelines’ za kanuni ambazo zinatumika.

“Sasa kabla hamjauliza kuhusu tafiti zao walizozifanya nyuma, mngefanya ‘research’ kwamba hizo tafiti zingine kama waliombea vibali na walipata.

“Kwahiyo tunasubiri watujibu na sisi tujiridhishe hizo sauti za wananchi nyingine kama waliombea vibali na walipata, kuwaandikia barua wadau wetu ni kawaida, ni njia ya kuwakumbusha,” alisema Zainab.

TWAWEZA

Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, kupitia ukurasa wa Twitter wa taasisi hiyo, alikanusha kuisambaza barua hiyo.

“Kama tulivyosema awali, tumepokea barua kutoka Costech na tunaifanyia kazi. Twaweza haijasambaza barua hiyo wala kuhusika kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii,” imesema taarifa hiyo.

Eyakuze alisema barua zote zinazopelekwa Twaweza huwekwa muhuri mbele ya aliyetumwa kuipeleka pamoja na risiti. “Barua inayosambaa mitandaoni haina muhuri wetu, tunaheshimu mawasiliano yote yanayofanywa na wadau wetu,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.