Biteko akamata shehena ya madini ya vito

Mtanzania - - Habari - MWANDISHI WETU -MOROGORO

NAIBU Waziri wa Madini, Dotto Biteko amekamata tani saba za Madini ya Rhodilite yanayotumika kutengeneza vito yakiwa yamefichwa nyumbani kwa mchimbaji wa madini hayo, Juvenal Mnene.

Mnene anadaiwa kuwa tangu alipoanza kujishughulisha na uchimbaji wa madini hayo mwaka 2013, amelipa mrabaha wa Sh 400,000 pekee serikalini.

Biteko aliyekuwa ameongozana na maofisa wengine wa wizara hiyo alikamata madini hayo nyumbani kwa mchimbaji huyo mkoani Morogoro na kuagiza vyombo vya sheria vimfikishe mahakamani.

Aidha, alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Gairo, Musa Mwakasula ashirikiane na Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, kuyapima madini hayo ili kujua kiasi halisi na kisha kumfikisha mtuhumiwa katika vyombo vya sheria.

Mchimbaji huyo ambaye ni mmiliki wa kampuni ya J. J. Mnene & Partners, alikamatwa katika ziara ya Biteko wilayani Gairo mkoani Morogoro yenye lengo la kukagua shughuli za wachimbaji wadogo wa madini ya vito na kutatua changamoto zao.

Baada ya kuwasili katika mgodi wa mchimbaji huyo uliopo eneo la Rubeho, Biteko alibaini kuwa mchimbaji huyo alikuwa amelipa mrabaha wa Sh 400,000 tu tangu mwaka 2013.

Hali hiyo ilimfanya Biteko kutaka kupewa taarifa ya uzalishaji na kiasi cha malipo yaliyolipwa serikalini ikiwa ni pamoja na kodi mbalimbali.

Mnene alimueleza Biteko kuwa, taarifa ya uzalishaji wa madini hayo na vielelezo vya malipo yaliyofanyika serikalini vipo nyumbani.

Kutokana na hali hiyo, Biteko na msafara wake alielekea nyumbani kwa Mnene ambapo alishuhudia madini ya vito aina ya Rhodilite yakiwa yamerundikwa kwenye chumba kimoja na kufungwa kwa kufuli bila kuwekwa lakiri (seal) ya Serikali kinyume na sheria ya madini inavyotaka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.