Matukio ya polisi kujiua yatafutiwe ufumbuzi

Mtanzania - - Tahariri -

KWA siku mbili mfululizo kumekuwa na matukio ya kusikitisha ndani ya Jeshi la polisi katika mikoa mbalimbali, ya kujiua kwa kujipiga risasi.

Matukio hayo pamoja na mengine kuelezwa sababu zake, yameibua maswali mengi.

Tukio la kwanza limetokea juzi mkoani Mara, ambako askari G 3777, Nelson William, anadaiwa kujiua kwa sababu za wivu wa mapenzi.

Taarifa zinaeleza kuwa kabla ya kuchukua uamuzi huo akiwa ndani ya kambi yake, aliacha ujumbe kuwa ameamua kujiua kwa sababu hana uhusiano mzuri na mpenzi wake ambao wamekuwa wakiishi wote.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki alisema askari huyo alikuwa na malumbano na mpenzi, ingawa yalionekana kuwa zaidi ya kimapenzi, jambo ambalo hata wao limewashtua.

Lakini pia mkoani Tabora nako askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), G. 8845 Konstebo Michael Hosea (29), amefariki dunia baada ya kujipiga risasi nne kwa kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Graifton Mushi, alisema tukio hilo lilitokea juzi.

Alisema askari huyo alifika mapema alfajiri kubadilishana zamu na wenzake waliokuwa lindo katika benki ya Access.

Muda mfupi baada ya kuchukua silaha alitoka kwenye chumba chao wanachotumia siku zote wawapo kazini na baadaye kujiua.

Tukio jingine kama hili limetokea Kidato mkoani Morogoro, ambako askari mwingine amejiua huku sababu zake bado hazijawekwa wazi.

Kiujumla matukio haya ni mabaya kwa sababu yamekatisha uhai wa askari ambao walikuwa ni muhimu kwa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Pia hayapaswi kuachwa yapite hivi hivi tukizangatia askari hawa wamepata mafunzo kwa gharama za Serikali na kula kiapo cha kulitumikia taifa kwa nguvu zao zote.

Matukio haya yote yanazua maswali kwamba kuna matatizo gani makubwa ambayo yanawapata askari wetu hadi kufikia hatua ya kujiua?

Ukiacha masuala ya mapenzi, inawezekana kuna matatizo ya msingi ambayo yanapaswa kutafutiwa ufumbuzi na mamlaka husika.

Tunasema hivyo kwa sababu askari wetu ni binadamu kama wengine, inawezekana kuna mambo ambayo wakati mwingine wanahitaji hata ushauri kutoka kwa wakubwa wao ambao tunaamini wako nao karibu kila siku. Kwa kufanya hivyo na kuzungumza nao kwa nia ya kutatua matatizo yao, kunaweza kuwa njia nzuri na mwafaka kuondokana na vifo hivyo.v Sisi MTANZANIA, kwanza tunampa pole Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro na familia zote kwa kuondokewa na askari hawa ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wanawategemea katika mambo mbalimbali.

Pamoja na pole hizi kwa IGP, tunamshauri ayaangalie kwa makini matukio haya ili kujua chanzo chake na kuyapatia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Pia tunawashauri makamanda wa polisi wa mikoa, wakuu wa polisi wa wilaya na wakuu wa vituo vyote kujenga utamaduni wa kuzungumza nao juu ya mambo mbalimbali, yakiwamo ya maisha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.