Walimu wapya msingi wanahitaji semina

Mtanzania - - Tahariri - Na MWANDISHI WETU DAR ES SALAAM

MWAKA jana, Serikali ilitangaza kuwahamisha walimu 7,463 wa ziada kutoka shule za sekondari kwenda kufundisha shule za msingi.

Takwimu za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), zilizotolewa Machi mwaka huu, zinabainisha kuwa shule za msingi nchini zina upungufu wa walimu 85,000 wakati ziada ya walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari ni 21,000.

Mikoa mbalimbali tayari imechukua hatua za kuwahamisha baadhi ya walimu kutoka shule za sekondari kwenda kufundisha msingi. Dar es Salaam na Mtwara ni miongoni mwa mikoa ambayo tayari imetekeleza agizo hilo.

Sasa basi, walimu hawa ambao wamehamishiwa katika shule za msingi, wanalazimika kujifunza mbinu mbalimbali zinazotumika msingi ili kuboresha ufundishaji katika vituo vyao vipya vya kazi.

Hii ni kwa sababu baadhi ya walimu waliohamishwa wamekumbana na changamoto mbalimbali na hivyo kuwakatisha wengine tamaa.

Walimu wengi wanasema mbinu zinazotumika kufundisha katika shule za msingi na sekondari ni tofauti, hasa ukizingatia kuwa mwaka 2016 mtaala ulirekebishwa hivyo ni vigumu kwa mwalimu mpya kuufahamu vema.

Licha ya kwamba walimu husika walipatiwa mafunzo, lakini bado kuna haja ya mafunzo hayo kufanyika mara kwa mara ili kuwajengea uzoefu na uelewa zaidi.

Jambo la muhimu ambalo haliwezi kupunguza ari ya walimu hao kufanya kazi kwa bidii ni kwamba maslahi yao yamebaki palepale, hakuna kilichopunguzwa zaidi ya kuhamishwa vituo vya kazi.

Malalamiko mengi yanayotolewa na walimu hao ni namna wanavyokumbana na misamiati migumu ya Kiswahili katika somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Hata hivyo, wapo walimu ambao tayari wamebaini upungufu uliopo, unaochangia baadhi ya watoto kumaliza elimu ya msingi wakiwa hawana uelewa wa kutosha, hivyo wanafanya kila jitihada kuhakikisha wanamaliza changamoto hiyo.

Uamuzi huu wa Serikali hakika ni mzuri, kwani una lengo la kuondoa pengo lililopo la walimu katika shule za msingi, jambo la muhimu ni kuwaelimisha waendane na mazingira mapya ya kazi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.