Walimu hawa wameteseka miaka 15

Mtanzania - - Mtazamo - NA BENJAMIN MASESE benjaminmasese@yahoo.com,0692925352

NITANGULIE kusema hongereni Kamati ya Shule ya Msingi Kanindo kwa uamuzi sahihi wa kuwaondoa walimu katika mazingira yasiyo rafiki. Nitakuwa mtu wa pili kuipongeza kamati hiyo baada ya Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola, ambaye amesema kamati hiyo kuwa ni mfano wa kuigwa.

Kilichofanywa na kamati hiyo ya Shule ya Kanindo iliyopo Kata ya Kishili, jijini Mwanza, ni kuwajengea ofisi walimu ambao tangu shule hiyo ianzishwe mwaka 2003, walikuwa wanakaa chini ya miti au kwenye ukuta wa jengo wanapotoka madarasani.

Wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja waliamua kutoa fedha zao mfukoni na kuanza kujenga ofisi hiyo bila kuwashirikisha wananchi, lengo likiwa ni kuonyesha uzalendo na uwakilishi wao ndani ya jamii iliyowaamini na kuwachagua kuisimamia taasisi hiyo.

Moja ya malengo waliyojiwekea kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ni siku 30, ambapo tayari shughuli hiyo imeanza, huku baadhi ya wadau wengine, wakiwamo viongozi wa kata na mitaa wakiunga mkono, huku naye Ofisa Elimu Mkoa, Ligola, akiahidi kuwa ataweka mkono wake katika ujenzi huo.

Kwa mujibu wa Ligola, kitendo cha kamati ya shule hiyo kujitolea wenyewe kimeonyesha utambuzi na ushirikiano wa karibu na Serikali katika kutatua changamoto kwenye sekta ya elimu.

Hali hiyo ya walimu kukaa chini ya miti imekuwa ikiwafanya kutotimiza majukumu yao ipasavyo, kwani ofisi iliyopo ya mwalimu mkuu ni ndogo na ndiyo iliyokuwa ikitumika kwa mambo yote, ambayo wakati wa kipindi cha mvua walimu hao wamekuwa wakilazimika kujibanza humo.

Licha ya walimu hao kufanya kazi katika mazingira magumu, wamekuwa wakijitahidi kufundisha vizuri wanafunzi na kufaulu kuendelea na masomo ya sekondari.

Hakika jitihada za kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Nyamhanga Mrimi na katibu wake ambaye ni Mwalimu Mkuu, Joseph Muli, zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote.

Wote tunatambua kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali, wananchi wanapaswa kujenga boma hadi kukamilika ambapo upande wa halmashauri unapaswa kuezeka.

Lakini kamati ya shule hiyo imeamua kutoa fedha zao mfukoni bila kuwachangisha wananchi, hivyo tunashauri Jiji la Mwanza kumalizia pale ujenzi wa boma utakapokamilika.

Hatua ya kamati hiyo kujitolea ilitokana na hivi karibuni Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Muli, kuitisha kikao cha dharura na kuelezea adha wanayopata walimu kipindi cha kiangazi na mvua. Alisema watumishi hao wanapata shida sana wanapotoka darasani.

Alidai kuwa, walimu wanalazimika kukaa kwenye ukuta wa madarasa kwa kufuata kivuli cha jua, kitendo ambacho kinawapa ugumu wa kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Alisema wakati wa mvua watumishi hao hujikusanya katika ofisi ya mwalimu mkuu ambayo nayo haitoshi.

Binafsi nawapongeza wajumbe wa kamati hiyo, ambao kwa dhamira ya dhati wameamua kuchanga kila mmoja kutoa tofali, saruji, nondo, mchanga, kokoto na vifaa vingine vitakavyohitajika wakati shughuli za ujenzi zikiendelea.

Nahitimisha kwa kuwaomba viongozi wa Jiji la Mwanza kuona umuhimu wa kutoa kipaumbele katika Shule ya Kanindo, hususan pale kamati hiyo itakapowasilisha ombi la kuezekwa kwa ofisi hiyo sambamba na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ambavyo ujenzi unatarajiwa kuanza baadaye.

Wote tunatambua kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali, wananchi wanapaswa kujenga boma hadi kukamilika ambapo upande wa halmashauri unapaswa kuezeka.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.