Ujio wa Dreamliner 787-8 ni mafanikio kwa Taifa

Mtanzania - - Mtazamo - NA MWANDISHI WETU

KABLA ya ujio wa ndege mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, kulikuwa na baadhi ya wanaharakati waliobeza kwa kusema kwamba ndege hiyo ni chakavu.

Hivi karibuni wakosoaji na wanaharakati hao waliumbuka baada ya ndege hiyo mpya kutua nchini na kupokelewa na mamia kwa maelfu ya Watanzania waliojitokeza kwenye mapokezi yake katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA).

Waliobeza na kukosoa kwamba ndege hiyo ni chakavu na wengine walisema haitaweza kutua endapo itaruka walipata aibu na wengi wao hawakuwepo kwenye mapokezi yake pale uwanja wa ndege.

Baada ya kuona juhudi zao zimeshindwa za kuchafua mafanikio haya ya Serikali ya Awamu ya Tano, wamegeuka na kutumia wataaalamu uchwara wa kwenye mitandao ya kijamii ili kuendelea na azma yao ya kukosoa na kujaribu kushawishi wananchi waone kuwa ndege hiyo haina tija na ni mzigo kwa Serikali.

Wakichangia baadhi ya wanaojiita wataalamu wa usafiri wa anga wa kwenye mitandao ya kijamii, wamediriki kuandika kwamba ndege iliyonunuliwa inapokuwa imeegeshwa tu kwa saa moja ni Dola za Marekani 30,000, lakini pia walikwenda mbali zaidi na kupotosha kuwa kila saa moja ndege hiyo itakapokuwa hewani itagharimu Dola za Marekani 17,000 mambo ambayo yote ni ya uongo.

Gharama zilizoainishwa na wakosoaji hao ni gharama ambazo hazipo kwa mujibu wa wataalamu wa usafiri wa anga duniani, hakuna gharama za namna hiyo na kama zingekua hivyo hakuna nchi ambayo ingeweza kumiliki wala kufanya biashara ya ndege kwani hata hao abiria kwa gharama hizo wasingemudu nauli za ndege.

Kwa mujibu wa wataalamu wa usafiri wa anga, gharama kubwa kwenye ndege ni za mafuta pamoja na matengenezo ambavyo kwa ujumla wake ni asilimia 65 ya gharama zote za uendeshaji wa ndege, asilimia 35, ndio matumizi mengineyo ikiwemo gharama za wahudumu, marubani, wahandisi, kulipia gharama za viwanja pamoja na gharama kidogo za maegesho, sasa kwa hali ya kawaida mtu akisema gharama za maegesho na kuruka ndio zinaifanya ndege hiyo mpya isilete tija anakuwa hana taarifa sahihi.

Wataalamu hao wamekwenda mbali zaidi kwa kufafanua kuwa ndege mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner, ndiyo ndege inayofanya vizuri kimataifa katika ulaji mdogo wa mafuta kwa asilimia 30 ukilinganisha na aina nyingine, hii inatokana na uwezo wake wa kuruhusu mwingiliano wa hewa ya oksijeni kusaidia katika kupunguza ulaji wa mafuta.

Aidha, malighafi iliyotumika kutengeneza ndege hiyo ni ya aina yake na si aluminum kama zilivyo ndege nyingine, hivyo kuifanya kuwa na uzito mdogo kunakowezesha pia kupunguza ulaji wa mafuta, hayo yote wakosoaji hawajayaelezea.

Ni vyema wanaotaka kuandika ama kuzungumzia masuala ya kitaalamu ya uendeshaji wa ndege na biashara hiyo, wawaone wataalamu husika ambao watawapa ufafanuzi na elimu juu ya uendeshaji wa biashara ya ndege, changamoto zake pamoja na takwimu sahihi.

Kwa taarifa tu za wataalamu wa uendeshaji wa biashara za anga ni kwamba, ni asilimia 3 tu ya mchango wa nchi za Afrika katika biashara ya usafiri wa anga duniani, hivyo waliopo kwenye biashara hiyo wanapoona nchi nyingine hasa za Afrika zinajitahidi kuingia kwenye soko hilo hawajisikii vyema wanaona ushindani utaongezeka, ndio maana wanalazimika kutumia kila mbinu chafu ikiwemo kutoa taarifa za uongo ili ionekane Tanzania haitaweza kuendesha biashara ya ndege. Yanapopatikana mafanikio kama haya ya kulifufua shirika letu la ndege, yanayoambatana na ununuzi wa ndege mpya ni vyema Watanzania tukaacha ushabiki na ukosoaji usio na tija na badala yake tusaidie namna bora ya kuweza kuendesha mashirika yetu wenyewe hususani shirika la ndege kwani ni utambulisho wetu kama taifa nje ya mipaka yetu.

Kwa mujibu wa wataalamu wa usafiri wa anga, gharama kubwa kwenye ndege ni za mafuta pamoja na matengenezo ambavyo kwa ujumla wake ni asilimia 65 ya gharama zote za uendeshaji wa ndege, asilimia 35.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.