Walia wake zao kuiba mazao kununua vipodozi

Mtanzania - - Kanda Ya Ziwa - Na MASYENENE DAMIAN

BAADHI ya wanaume katika Kijiji cha Mwanangwa Kata ya Mabuki wilayani Misungwi, wamelalamikia tabia ya wake zao kuuza mazao kinemela ili kununua vipodozi na urembo mwingine.

Wamesema hali hiyo imekuwa ikisababisha mfarakano, usaliti na umaskini wa katika ndoa na familia.

Madai hayo yalitolewa baada ya wanawake kudai kutelekezwa na waume zao wakati wa mavuno kwa kuchukua fedha za mauzo ya mazao na kwenda kula raha na wanawake wanaofanya ukahaba kutoka Mwanza ambao wamepewa jina la nzige.

Walikuwa wakizungumza juzi kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwanangwa wakati wa mdahalo maalumu kujadili jinsi kipindi cha mavuno kinavyokuwa na changamoto wilayani humo.

Mdahalo huo uliandaliwa na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini.

Ilielezwa kuwa wakati wa mavuno ya nafaka mbalimbali wakulima huuza mazao yao na kupata mamilioni ya fedha, ndipo migogoro inapoibuka kutokana fedha za mauzo.

Mmoja wa wanaume waliochangia kwenye mdahalo huo, Mussa Kiyumbi, alisema chanzo cha migogoro na hata kupigwa kwa wanawake katika ndoa ni kutokana na kuwanyima unyumba waume zao lakini pia huuza mazao ya familia kinyemela.

“Wanawake hawa wanauza mazao kinyemela kwa lengo la kwenda kununua vipodozi ambavyo waume zao hawavijui.

“Wanabeba mazao kidogokidogo kwenye ndoo na kwenda kisimani kama wanaofuata maji kumbe wanauza mazao, mwanaume haujui, mwisho wa siku unakuta mavuno yanapungua.

“Changamoto nyingine tukidai haki zetu za ndoa wake zetu hawaridhii ndiyo maana tunatoka nje kutafuta suluhu na kupoza hasira kwa nzige,” alisema.

Naye Andrew Mabuga, licha ya kukiri kuwa asilimia 75 ya migogoro hiyo kijijini hapo husababishwa na wanaume, alisisitiza kuwa wanawake wengi hupenda kuiga maisha ya marafiki zao kwenye vikundi na kuthamini sherehe ambazo huzidi kuwaletea umaskini.

Regina Kubunga, alisema wanawake wengi wamekuwa wakiamua kuuza mavuno ya akiba ili kumudu gharama mbalimbali kutokana na wanaume kuuza na kumalizia fedha zote kwenye anasa na ulevu.

Alisema wanaume wanakuwa wakichochea wanawake kuiba nafaka kwani hata baada ya kuuza mazao wanapoomba fedha za matumizi wamekuwa wakijibiwa ‘tumia akili yako’.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwasonenesha wanawake na baadhi kuanza mgogoro na wanaume wao.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, aliwataka wananchi kuyatumia vizuri mavuno kwa kuimarisha familia zao na kujiletea maendeleo katika kaya zao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Eliurd Mwaiteleke, aliwataka watendaji wa vijiji na vitongoji 31 vya Kata hiyo yenye wakazi 17,000 kuwajibika ili watoto wapate haki ya kusoma.

– PICHA:DERICK MILTON

USAJILI: Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson, akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Simiyu mjini Bariadi jana, kutathimini utekelezaji wa mpango wa usajili wa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano mkoani humo. Kushoto ni Katibu Tawala wa mkoa huo, Jumanne Sagini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.