Serikali yatoa Sh bilioni 1.5 kukamilisha hospitali Ilemela

Mtanzania - - Kanda Ya Ziwa - Na PETER FABIAN

MBUNGE wa Ilemela, Angelina Mabula (CCM) amesema serikali imetoa Sh Biloni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.

Alikuwa akizungumza juzi kwenye mikutano ya hadhara katika Kata za Buswelu na Kahama kwa nyakati tofauti.

Mabula alisema kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela ilikwisha kujenga jengo la kupokea wagonjwa wa nje (OPD), fedha hizo zitatumika kuongeza majengo ya utawala, wodi, maabara, utabibu, chumba cha upasuaji na cha kuhifadhia maiti.

“Wakati tukiendelea na ujenzi wa hospitali ya wilaya pia tumepata Sh milioni 400 za kuongeza majengo ya kutolea huduma mbalimbali na kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya cha Buzuruga, Zahanati ya Ibinza, Lukobe zitakazogharimu Sh milioni 300 huku Sh milioni 100 zikiwa ni kwa ajili ya kununulia vifaa tiba,” alisema.

Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, alieleza kuwa serikali imekwisha kukamilisha kuboresha Kituo cha Afya Karume ambacho kimeongezewa majengo ya kutoa huduma mbalimbali ikiwemo chumba cha kuhifadhiwa maiti.

Alisema hivi sasa kituo hicho kinaendelea kutoa huduma kwa wananchi wa kata za Kayenze na Bugogwa wakati Kituo cha Afya Sangabuye nacho kinaendelea kuhudumia wananchi ukanda huo.

Aliwahakikishia wananchi ambao maeneo yao hayajapata umeme kuwa wako katika mpango wa REA III na tayari Tanesco na mkandarasi wako kwenye baadhi ya mitaa wakiendelea kutekeleza mradi huo.

Hata hivyo alisema zimekuwapo changamoto za wananchi kutaka kulipwa fidia wakati tayari imekwisha kutolewa elimu na kukubaliana kuachia maeneo yao ili kupitishwa nguzo za umeme.

“Tuwe tayari kuipokea miradi ya Serikali na mara nyingine kuomba fidia ni kuchelewesha kupata huduma.

“Lakini tutatumia busara kwa kulipa fidia endapo tutatakiwa kufanya hivyo lengo ni kuharakisha maendeleo na huduma kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamevumilia ikilinganishwa na ukubwa wa majukumu ya serikali,” alisema.

Mabula aliwaeleza wananchi hao kuwa i Halmashauri ya Ilemela imepata miradi 15 ya ujenzi wa barabara nne za lami na 11 za kiwango cha changarawe .

Alisema ujenzi huo unaendelea kutekelezwa na TARURA ambako kwa sasa wakandarasi wako kazini.

Mbunge huyo alisema hadi kufika mwaka 2019 hali ya miundombinu katika mitaa ya kata 19 ya jimbo hilo itakuwa ikipitika kwa urahisi zaidi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.