NSSF kuwafikia wananchi wengi zaidi

Mtanzania - - Mkoa Tangazo - Na GUSTAPHU HAULE

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii wa Taifa (NSSF), umeanzisha mpango maalumu wa kuhakikisha wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi, wanapata fursa ya kujiunga na mfuko huo ili waweze kufaidika na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Mpango huo umetambulishwa juzi mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibishaji wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Isiyo Rasmi, Mariam Muhagi, katika semina ya siku tatu.

Semina hiyo, iliwakutanisha viongozi wa vikundi vya ushirika na wasiokuwa katika ushirika katika Mkoa wa Pwani chini ya uratibu wa NSSF.

Katika maelezo yake, Muhagi, alisema lengo la semina hiyo ni kutoa elimu ya umuhimu wa mfuko wa hifadhi ya jamii kwa wajasiriamali na wananchi wengine waliopo katika sekta isiyo rasmi.

“Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Bunge, mwaka huu limepitisha sheria mpya namba mbili inayoboresha hifadhi ya jamii nchini na sheria hiyo inatoa nafasi ya kuiacha mifuko miwili ukiwamo NSSF.

“Mambo muhimu yaliyopo katika sheria hiyo ni pamoja na msisitizo wa kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa kuwafikia Watanzania wote wakiwamo wale waliojiajiri wenyewe,” alisema Muhagi.

Naye Meneja wa NSSF, Mkoa wa Pwani, Linus Bwegoge, alisema kwa sasa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kwa wakati kwa kuwa kamati maalumu imeshaundwa ili kuhamasisha vikundi na ushirika kujiunga na mfuko huo.

“Katika Mkoa wa Pwani, tumeanza kutoa elimu ya umuhimu wa hifadhi za jamii kwa viongozi wa vikundi na ushirika 50 na wale wasio katika ushirika zaidi ya 35.

“Baada ya hapo, viongozi hao watatumia fursa hiyo kuwahamasisha wenzao ili nao wapate maarifa kama waliyoyapata.

“Kwa hiyo, wajasiriamali wa vikundi mbalimbali waliopo mkoani kwetu Pwani, tumieni fursa hiyo kikamilifu ili muweze kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili,” alisema Bwegoge.

Tumeanza kutoa elimu ya umuhimu wa hifadhi za jamii kwa viongozi wa vikundi na ushirika 50na wale wasio katika ushirika zaidi ya 35. -Linus Bwegoge

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.