Mpinga ashuhudia ubunifu banda la Veta

Mtanzania - - Habari Za Sabasaba -

ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga, jana ametembelea banda la Mamlaka ya Elimu ya Ufundi (Veta), kushuhudia teknolojia mbalimbali ambazo zimebuniwa na walimu kwa ushirikiano na wanafunzi.

Miongoni mwa gunduzi hizo ni pamoja na mashine ya kukausha mazao, mfumo wa kuzima taa hata kama upo mkoa mwingine na ule wa kuwasha bodaboda kwa kutumia kofia ya abiria na dereva.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda hilo, Mpinga, alikipongeza chuo cha Veta kwa kubuni mifumo ya kisasa yenye gharama nafuu ambayo itasaidia kuikomboa jamii.

Mpinga alishauri teknolojia hizo ziongezewe zaidi utaalamu ili kuifikia jamii sehemu kubwa.

Mpinga alisema katika zama hizi za kuelekea uchumi wa viwanda ni vyema jamii ikashirikishwa ili tekonolojia hizo mpya zienee kwa kasi hasa katika maeneo ya vijijini.

Akizungumzia mfumo huo wa uwashaji pikipiki mwanafunzi Rentius Pesha, alisema mfumo huo husaidia kutokomeza ajali za kizembe na wizi.

“Tunaiomba Serikali itunge sheria ya kutaka pikipiki zote kwenda Veta ili kufungwa mfumo huo ambao utasaidia kukabiliana na athari kichwani pindi ajali zinapotokea,” alisema Pesha.

Pikipiki hiyo iliyopo katika viwanja ya maonyesho ya 42 ya biashara, imewekwa kifaa maalumu na kwenye kofia za pikipiki.

Alisema lengo la kubuni mfumo huo ni kubainisha teknolojia si lazima itoke nje ya nchi bali mamlaka hiyo ina uwezo wa kuvumbua teknolojia mbalimbali ikiwemo kusaidia kuokoa nguvu kazi ya taifa kwa kuanzia na kuokoa wanaopata matatizo vichwani.

“Ajali inapotokea na kuumia kichwani, mtu hushindwa kufanya jambo lolote, lakini akiumia kiungo kingine anaweza kufanya jambo lolote hivyo kwa kubaini kuwa waendesha bodaboda huvaa kofia kwa kuogopa polisi na si kujilinda tukaona bora kutafuta suluhisho,” alisema Pesha.

Mwalimu katika chuo hicho cha Kipawa, Anneth Mganga, aliiomba Serikali kutunga sheria katika kutumia mfumo huo kwa kusaidia kupunguza nguvukazi nyingi iliyopo hospitalini kutokana na kuumia vichwani na pikipiki.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.