Meli ya Freedom: Jiji la kwanzalinaloelea majini

Mtanzania - - Kisima Cha Ujuzi - JOSEPH HIZA NA MTANDAO

NI jiji la wakati ujao, ambalo litahitaji ubebe mabegi yako kuelekea baharini, iwapo Kampuni ya Freedom International ya Florida nchini Marekani itakamilisha wazo la kulijenga.

Mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 10 sawa na Sh trilioni 22 za Tanzania, utatoa fursa kwa abiria uzoefu wa kuishi baharini.

Kampuni hiyo ina matumaini ya kujenga meli hiyo yenye urefu wa futi 4,500, upana wa futi 750 ukiwa na kila kitu pamoja na uwezo wa kuhifadhi wenyeji 50,000.

Meli hiyo itatoa elimu kwa watoto wa shule za awali pamoja na huduma za afya kwa watu wa rika zote.

Abiria watafurahia kila kitu wanachoweza kukikuta katika majiji makubwa duniani kama vile casino, wilaya ya kibiashara, makumbusho ya sanaa.

Kadhalika kuna bwawa la samaki, shule, hospitali, bustani, kiwanja cha ndege kitakachokuwa juu kabisa ya paa la meli hiyo na mengine mengi.

Wageni na wenyeji wana uwezo wa kuondoka na kuingia kwenye jiji hili linaloelea kwa ndege au boti.

Wabunifu wa wazo hilo wametoa picha za kompyuta za kile wanachoamini meli hiyo itakavyokuwa pindi itakapokamilika.

Mkurugenzi na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Freedom Ship International, Roger M Gooch, anasema hiyo itakuwa ndio meli kubwa kuwahi kujengwa, na jiji la kwanza linaloelea kwenye maji.

Meli hiyo inayotegemea kuwa na ghorofa 25, itakuwa na uwezo wa kuwapa makazi ya kudumu mbali ya watu 50.000, pia nafasi za ziada ya kupokea wageni wengine 30.000.

Aidha, kuna makazi 20,000 ya wafanyakazi wa meli, na mengine 10,000 kwaajili ya wageni watakaopitisha usiku mmoja.

Meli hiyo inatazamiwa kuizunguka dunia nzima nchi moja hadi nyingine, bara moja hadi lingine na itafika hadi Afrika, na haitakuwa ikikaa sehemu moja kwa muda mrefu.

Uwanja wa ndege utakaokuwa juu ya meli utakuwa kwa namna ya kuwezesha ndege kuruka na kutua hata wakati meli ikiwa inatembea majini. Na itakuwa ikitumia umeme wa jua na nishati ya upepo.

Ukubwa wa jiji hili linaloelea ambalo kama tulivyoona pamoja na mambo mengine litakalokuwsa na urefu wa futi 4.500 ni mara nne ya ule wa meli ya kifahari ya Queen Mary II yenye urefu wa 1.132.

Wazo la kuanzisha meli hiyo lilibuniwa mwishoni mwa miaka ya 1990.

Awali Gooch, alisema kampuni yake inajaribu kukusanya kiasi cha dola bilioni sita zinazohitajika kuifanya ndoto hiyo iwe kweli, ambayo ni mpango wake uliopo kwa miaka mingi.

Hata hivyo, pamoja na kutangazwa sana kwa mradi huo ikiwamo katika majarida maarufu kama Newsweek, na kutangazwa redioni na kipindi cha televisheni ikiwamo cha wahandisi, mradi huo umepiga hatua kidogo

Awali ulikuwa uanze kujengwa mwaka 2001, lakini haujaanza kufikia sasa ijapokuwa wazo bado liko pale pale.

Ukiwa umepangwa kutumia dola bilioni sita mwaka 1999 kufikia mwaka 2002 gharama ziliongezeka kuwa dola bilioni 10 na Julai 2008 taarifa kwa vyombo vya habari ikaeleza kuchelewa kuanza kunatokana na ugumu wa kupata fedha.

Novemba 2013, kampuni hiyo ikatangaza kwamba mradi huo unafufuliwa, ijapokuwa hadi sasa bado haujaanza kwa kinachoonekana tatizo la fedha.

Wazo hilo pia limeandikiwa kitabu na mwandishi mashuhuri Jules Verne katika riwaya yake ya Propeller Island.

Lengo kuu la mradi huo pamoja na mambo mengine ni kuwezesha watu kuweka akiba ya fedha zao dhidi ya kutozwa kodi.

Ndege ikiruka kutoka Meli ya Freedom

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.