Mbio za urais, kiu na matumaini ya wananchi

Mtanzania - - Kisima Cha Ujuzi - Na MARKUS MPANGALA

PROFESA T.L Maliyamkono aliandika kitabu cha ‘The Race for the Presidency; The First Multiparty Democracy in Tanzania.’ Hii ilikuwa ni mwaka 1995 kabla ya uchaguzi mkuu wa urais, wabunge na madiwani. Kilichapishwa na Tanzania Publishing House Limited ya Dar es Salaam na kupewa nambari ISBN 9987-25008-4.

Sura ya kwanza anazungumzia suala la rushwa na ukwapaji wa kodi, mwisho wa misaada, mashirika ya kifedha ya kimataifa na mengineyo. Sura ya pili anazungumzia maendeleo ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mwandishi anazungumzia taswira ya CCM, kuibuka kwa vyama vingine, vita ya kuwania madaraka iliyozaa ombwe la uongozi, uongozi wa Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi, hadhira na hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, taswira za waliogombea urais, sababu za kuathirika mchuano wa urais.

Sura ya tatu anaanza kwa kuzungumzia umahiri wa Nyerere katika siasa, mafanikio na kushindwa kwake. Sura ya nne anazungumzia matatizo ya wakimbizi yanayoathiri mbio za urais.

Sura ya tano anaeleza madhara ya nchi kuwa njia panda kutokana na utegemezi wa misaada kutoka nje, nani alifaa kuwa mgombea urais wakati ule, elimu, afya, utawala bora, mgawanyo wa madaraka, kilimo, nafasi ya mashirika ya umma na mgawanyiko wake, elimu ya uraia na siku 200 usiku na mchana za kukosa usingizi.

Mwandishi anatufahamisha juu ya kufungwa kwa baadhi ya matawi ya benki kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Anajadili suala la uchumi kama ajenda kuu ya uchaguzi ya mwaka 1995.

Anasema matawi 18 ya benki hiyo yalifungwa kutokana na hali mbaya. Anasema mijadala ya uchumi ilishika kasi nchini. Watu walijadili hali zao .... Lakini wengine walikuwa kwenye vita kali ya kuwania madaraka.

“Uhaba wa ajira ulichochewa na mashirika ya misaada ya nje yaliyopendekeza mabadiliko ya sera, viwanda vilikuwa ovyo, huduma zilikuwa duni. Huduma za jamii ziliporomoka, maji, afya, elimu na barabara pamoja na ushirikiano uliokuwapo bado haukutatua tatizo la msingi,

“Sababu za nje ziliendelea kuwa dhaifu huku kiwango chetu cha uuzaji wa bidhaa nje kilikuwa kidogo, theluthi ya bidhaa zilizosafirishwa kuingia nchini na maendeleo ya uchumi vilibaki kuwa tatizo kwa sababu ya utegemezi. Matokeo yake serikali ilihitaji sapoti kubwa ya bajeti yake au kutegemea mikopo ya nje ili kuziba nakisi. Wakati huo sekta ya viwanda iliendelea kuwa dhaifu huku mashirika 400 ya umma yakiwa na uzalishaji mdogo.” (uk.1).

Pia anasimulia msuguano uliokuwapo kati ya Serikali na Bunge, kwamba kulikuwa na uhusiano mbaya kati ya mihimili hiyo kwa kila upande kutunisha misuli yake.

Suala la afya, anasema hospitali hazikuwa na dawa za kutosha (Muhimbili). Watu waliishi kwa chakula cha msaada kutoka Japan hususani wali. Mashirika ya umma yalikuwa na uzalishaji hafifu. Nchi ilikabiliwa na mzigo wa madeni makubwa kiasi kwamba watu walikuwa wakijadiliana namna gani rais mpya angeweza kuiondoa nchi kwenye ulimbo wa madeni.

Anasema watumishi wa umma walitendwa kana kwamba hawakuwa sehemu ya ujenzi wa uchumi wa nchi. Ushiriki wa watumishi wa umma ni muhimu na wanapaswa kupewa ujuzi kila mara.

Anakumbusha kuanguka kwa Benki ya Meridian pamoja na Benki ya Nyumba kuzabwa makofi ya madeni kila kukicha. Shirika la Taifa la Usagaji likazingirwa na uzalishaji mdogo. Tanzania ikapewa nyongeza ya msaada wa bajeti kukabiliana na wakati mgumu.

Mwaka 1994 wahisani Norway, Sweden na Umoja wa Ulaya ziliondoa misaada yao, kisha Uholanzi ikafuatia. Sababu kubwa ni kushindwa kukusanya mapato, rushwa na upendeleo. Magonjwa kama Ukimwi, kipindupindu, malaria na ebola yaliweka kambi nchini.

Mwandishi anaelezea juu ya mauzo ya ekari 380,000 za Loliondo. Anasema suala la rushwa linatengeneza matabaka miongoni mwa jamii kwakuwa linachochea ongezeko la ukiukwaji wa sheria na taratibu zilizopo.

Anasema hilo ni kwamba viongozi wanatumia nafasi zao kujinufaisha badala ya kuunufaisha umma. Rushwa pia iliwakasirisha wahisani ambao waliamua kuikimbia nchi yetu.

“Uchumi wa Tanzania unatakiwa kujengwa nyumbani. Uchumi wenye nguvu hauwezi kuendeshwa kwenye jamii isiyoimarika wala inayotanguliza rushwa, au isiyokuwa na uwezo wa kutanua milango ya uwekezaji.” (uk.9).

Mwandishi anaelezea suala sugu la kutegemea mashirika ya mikopo na misaada. Anasema dunia inabadilika na utegemezi wa Tanzania kwa misaada ya nje unazidi kuota mizizi na kuzalisha matatizo mengi.

Anasema Tanzania inapaswa kusimama kwa miguu yake kwenye suala la viwanda na biashara ili kuzalisha bidhaa na kusafirisha nje kwa uhakika.

Aidha, anaeleza kuwa kilimo ni miongoni mwa maeneo yanayoinufaisha nchi yoyote yenye fursa hiyo. Anasema rasilimali watu zisimamiwe, elimu stahiki itolewe, maliasili, mashirika ya umma viwe chagizo la ukuaji wa uchumi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.