Chidya; Sekondari iliyokombolewa kutoka hali hatarishi Masasi

Mtanzania - - Kisima Cha Ujuzi - Na ASHA BANI ALIYEKUWA MASASI

SHULE ya Sekondari ya Chidya iliyopo wilayani Masasi mkoani Mtwara, ilianzishwa mwaka 1929. Awali shule hii ilikuwa ikikabiliwa na matatizo ya uchakavu wa miundombinu na maji safi.

Tangu kuanzishwa kwake, wanafunzi wamekuwa wakitembea mrefu kufuata maji mtoni kwa ajili ya matumizi ya kunywa, kufua, kupikia na usafi wa mazingira.

Shule hiyo ya wavulana, sasa imetatua changamoto hizo kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), unaosimamiwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Mradi huu umekarabati mabomba na kuvuta maji shuleni hapo, mbiundombinu ya shule imeboreshwa na hivyo kuwafanya wanafunzi kusoma kwa amani.

Aklei Baila mwanafunzi wa kidato cha tano shuleni hapo, anasema alipojiunga na shule hiyo alihisi ni kama ametelekezwa kwa kuwa hapakuwa na majengo mazuri na suala la kutembea mwendo mrefu kutafuta maji lilikuwa likimkwaza.

Anasema ilimlazimu kutumia

siku nzima kutafuta maji badala ya kujisosmea, na hata akiwahi kurudi anakuwa amechoka.

“sasa hivi mambo yamebadilika hata muda wa kujisomea tunapata, na majengo tuliyonayo yanavutia kutamani kubaki darasani,’’ anasema Baila.

Anasema hata wazo alilokuwa nalo la kutaka kuhama shule sasa hivi halipo tena.

Naye Said Mnguvu, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, anasema awali wanafunzi wengi waliku wakifika shuleni hapo hawakai muda mrefu wanahama shule, lakini sasa hivi suala hilo halipo.

Anasema hata walimu walikuwa hawapendi kuendelea kufundisha kwa sababu ya mazingira mabaya ya shule, hivyo wanafunzi hawakuwa wakifanya vizuri darasani.

Anasema kuna wakati walimu na wanafunzi walikuwa wakichanganyika na kuanza kusaka maji, hivyo haikuwa rahisi kufahamu mwalimu ni yupi na mwanafunzi ni yupi.

Hivyo basi, mradi huo umewasaidia hata kukaa vizuri darasani, ambapo awali walikuwa wakijirundika katika madarasa machache yaliyokuwapo. Hata walimu nao hawakuwa na ofisi.

“Licha ya majengo kuwa chakavu, pia madarasa yalikuwa hayatoshi, mabweni machache, maabara haikuwapo na hata ofisi za walimu hivyo, kuwafanya walimu kutumia vymba vya madarasa kama ofisi,” anasema.

Mmoja wa wazazi wa wanafunzi na washiriki wa maendeleo ya shule hiyo, George Kapondo, anasema wanaishukuru serikali kwa ujenzi huo kwani hata wao walikuwa wanakosa amani kuona watoto wao wakisomea katika mazingira hatarishi.

“Ni jambo la kuishukuru Serikali, watoto wetu walikuwa wakisomea kwenye mazingira hatarishi. Hawakuwa na majengo mazuri, yaliyokuwapo yalikuwa ni ya zaidi ya 30 iliyopita, hivyo yalichakaa kupita kiasi,” anasema Kapondo.

Mkuu wa shule hiyo, Zawadi Mdimbe, anasema kuwa mradi wa EP4R umewasaidia kuboresha miundombinu ambayo kwa sasa inavutia walimu na wanafunzi.

Anasema walipatiwa Sh milioni 400 ambazo zimewasaidia kukarabati miundombinu ya maji, kuvuta maji shuleni na kufunga mabomba maeneo mbalimbali ya shule.

Anasema sasa hivi kasi ya wanafunzi kutaka kuhama shule imepungua na badala yake wengi wanataka kuhamia.

Anasema walimu nao wamekuwa na ari ya kufundisha tofauti na ilivyokuwa awali.

Naye Diwani wa Kata ya Chiwata, Jofrey Bakari anasema hatua hiyo ya serikali kuwanufaisha Masasi ni ya kupongezwa kwani awali shule ilikuwa na hali mbaya.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chidya

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.