Trump atishia kuiondoa Marekani NATO

Mtanzania - - Habari Za Kimataifa / Matangazo -

RAIS wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuiondoa nchi yake kutoka Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi (NATO), iwapo nchi za Ulaya hasa Ujerumani, Ubelgiji na Hispania hazitaongeza bajeti zao za ulinzi.

Trump ameendeleza kauli kali dhidi ya washirika wanaounda NATO, akisema marais wengi wa Marekani walikuwa wakijaribu bila mafanikio kwa miaka mingi kuilazimisha Ujerumani na nchi nyingine tajiri za NATO kuongeza bajeti za ulinzi.

Amesema kutokana na nchi hizo kutoongeza bajeti kumeifanya Marekani pekee ibebe mzigo wa mabilioni ya dola kwa ajili hiyo.

Rais Trump amesisitiza nchi hizo zitenge asilimia nne ya pato la jumla la nchi zao katika bajeti ya ulinzi, akidai Marekani inatumia mabilioni ya dola kuziba pengo la Ulaya.

Trump amechukua msimamo wa kibabe katika mkutano huo wa kilele wa NATO akihoji thamani ya muungano huo, ambao umekuwa ukiielekeza sera ya nje ya Marekani kwa miongo kadhaa na kuwamulika washirika wake pamoja na kupendekeza ongezeko kubwa la matumizi ya kijeshi katika nchi za Ulaya.

Trump pia alikabiliwa vilivyo na nchi za Ulaya kwa kumkumbatia Rais Vladimir Putin wa Urusi lakini akaigeuzia kibao Ujerumani.

Katika hilo alimulika uhusiano wa nchi hizo akidai Serikali ya Kansela Angela Merkel imejiachia na kudhibitiwa kikamilifu na kutekwa nyara na Urusi kutokana na maslahi ya kutaka bomba la gesi asilia kutoka Urusi.

Amedai Ujerumani imeanza kuilipa Urusi mabilioni ya fedha kwa ajili ya mahitaji yao ya nishati kutoka bomba la Urusi, na hilo ni jambo lisilokubalika, kauli ambayo imepingwa vikali na Merkel.

Wakosoaji wanahisi mlolongo wa kauli mpya za Trump na hasa za kulazimisha nchi wa Ulaya ziongeze kiwango cha bajeti ya ulinzi zinatishia kuibopmoa jumuiya hiyo ya miongo kadhaa iliyoanzishwa kwa lengo la kukabiliana na uchokozi wa uliokuwa Muungano wa Sovieti wa Urusi (USSR).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.