Vita ya kinda Chilunda dhidi ya mkongwe Kagere

Mtanzania - - Habari Za Michezo - Na MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM

TIMU za Simba na Azam FC leo zitashuka dimbani kuumana katika mchezo wa fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hizo zitaingia uwanjani kuumana, huku kila moja ikiwa inajiamini kiasi cha kutosha baada ya kushuhudiwa zikifika hatua hiyo pasipo kupoteza mchezo hata mmoja.

Kwa kuanza na Simba, ilizindua kampeni zake kwa kuiangamiza timu ya Dakadaha 4-0 ya Somalia, ikaitungua APR mabao 2-1, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na ndugu zao wa Singida United, ikaisambaratisha Ports ya Djibouti bao 1-0 kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 juzi dhidi ya JKU ya Zanzibar.

Kwa upande wa Azam, heka heka zake zilianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kator ya Sudan Kusini, ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Vipers ya Uganda, ikaikaanga JKU ya Zanzibar mabao 2-1, ikaisambaratisha APR ya Rwanda mabao 4-2, kabla ya juzi kuidungua Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0.

Mara ya mwisho Simba na Azam zilikutana Februari 7 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 37 na mshambuliaji, Emmanuel Okwi.

Hii ina maana kwamba, timu hizo zinapokutana leo, Simba itaingia uwanjani ikilenga kuendeleza rekodi ya ushindi dhidi ya Azam, lakini Azam itataka kulipa kisasi cha kupoteza mchezo Februari 7.

Katika michuano ya Kagame, Simba ndio kinara wa kutwaa taji hilo mara nyingi zaidi ikifanikiwa kubeba mara sita, leo itakuwa inafukuzia taji la saba.

Azam kwa upande mwingine, inamiliki taji moja la Kagame ililolibeba mwaka 2015, hivyo itaikabili Simba leo ikisaka rekodi mpya ya kusaka taji la pili. Mshambuliaji, Meddie Kagere, ni wazi ataendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ya Simba, huku akitarajiwa kuwa mchezaji atakayechungwa zaidi kama itakavyokuwa kwa Shaaban Idi ‘Chilunda’ wa Azam ambaye amekuwa katika kiwango bora katika michuano hiyo akifanikiwa kuongoza chati ya wafungaji akiwa ametupia mabao saba mpaka sasa.

Safu za ulinzi zinatarajia kuongozwa na wachezaji wenye uzoefu kwa pande zote, Aggrey Morris hakuna mashaka atakuwa kiongozi kwa wachezaji wenzake wa eneo hilo kama ambavyo Pascal Wawa amekuwa akiaminiwa Simba.

Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Masoud Djuma, amesema wanaiheshimu Azam hasa kutokana na ubora iliouonyesha katika michuano hiyo mpaka sasa, lakini anaamini vijana wake hawatamwangusha kwa kuhakikisha wanapeleka ubingwa Msimbazi.

Lakini Kocha Mkuu wa Azam, Hans van der Pluijm, amesisitiza dhamira yao ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo.

- PICHA: JUMANNE JUMA

KWANJA: Mchezaji wa Simba, Rashid Juma, akimruka mchezaji wa JKU, Edward Peter Mayunga, katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Kagame uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam juzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.