Chadema yaanza kulia rafu uchaguzi mdogo

Mtanzania - - Mbele - Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

WAKATI uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma ukitarajiwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelalamikia kuanza kuchezewa rafu.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika katika Kata 79 zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini. Tayari Chadema kimempitisha Elia Michael kugombea ubunge Buyungu.

Akizungumza makao makuu ya chama hicho jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji alisema wameanza kuchezewa rafu katika Halmashauri ya Tunduma mkoani Songwe na Halmashauri ya Kilolo mkoani Iringa.

“Mchakato ndani ya chama ulifanyika kuhakikisha tunapata wagombea madhubuti, imara na makini watakaotuwakilisha katika uchaguzi huu lakini kuna mtanziko katika Halmashauri ya Tunduma na Kilolo.

“Katika hatua za mapema kabisa kumeanza kuonekana huu uchaguzi utavurugwa na baadhi ya viongozi ambao hawajiamini,” alisema Dk. Mashinji.

Kwa mujibu wa Dk. Mashinji, mgombea wao wa udiwani katika Kata ya Kwakilosa mkoani Iringa, Godfrey Mfyagila usiku wa kuamkia jana alivamiwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake na kunyang’anywa fomu.

Alisema katika Halmashauri ya Tunduma walifanya mchakato wa kuwapata wagombea wa kata tano lakini walishangaa kutaarifiwa kuwa tayari kuna barua ya kutambulisha wagombea imepelekwa kwa mkurugenzi ambayo alidai kuwa imegushiwa kwani haiko kwenye mfumo wa barua za Chadema.

Aidha, Dk Mashinji aliwataja wagombea waliopitishwa na chama hicho na kata zao kwenye mabano kuwa ni Osia Kibwana (Kaloleni), Boniface Mwakabanje (Majengo), Elia Lonje (Songea), Ally Sinkolongo (Mpemba) na Hitla Haonga (Mwakakati).

“Mkurugenzi alikataa barua ya katibu wa wilaya ya kuwatambulisha wagombea waliopitishwa na chama, mimi nikaamua kuandika barua nikamtumia katibu wa kanda ampelekee, lakini alikataa akasema anatambua barua ya awali aliyodai imeletwa na katibu wa jimbo wakati si kweli,” alisema.

Kutokana na madai ya rafu hizo alisema wameripoti suala hilo polisi kwa sababu kughushi ni jinai na kwamba tayari wameandika barua kwa mkurugenzi wa uchaguzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kumtaarifu huku wakitaka uharaka wa kulitatua. NEC Akizungumza na MTANZANIA kuhusu madai hayo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Athumani Kihamia alimtaka Dk. Mashinji awasilishe barua ya kuwatambulisha wagombea waliopitishwa na chama hicho NEC ili kuondoa migogoro.

“Kama wanadai hiyo barua ni feki basi walete mpya na iletwe na katibu mkuu mwenyewe kwa sababu tulishatoa maelekezo ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara,” alisema Dk. Kihamia.

– PICHA: FIDELIS FELIX

MNAONA?: Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, akionyesha orodha yenye jina la mgombea ubunge Jimbo la Buyungu na wagombea wa kata waliopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho, Dar es Salaam jana.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.