Bodi ya Mikopo yaongeza muda kwa wanafunzi elimu ya juu

Mtanzania - - Mbele - Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangza kuongeza muda wa wiki mbili kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 na kuwataka kuyatuma kwa njiaya mtandao.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru ilieleza kwamba tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi kupitia mtandao wa HESLB (https://olas. heslb.go.tz), itakuwa Jumanne, Julai 31, mwaka huu.

“Aidha, tarehe ya mwisho ya kutuma nakala ngumu kwa ‘EMS’ kupitia Shirika la Posta Tanzania (TPC) ni Jumanne, Agosti 14, 2018 ili kutoa nafasi kwa HESLB kuchambua, kuhakiki na kupanga mikopo kwa waombaji wenye sifa.

“Hatua hii inalenga kutoa fursa kwa waombaji wa mikopo ambao hawajakamilisha nyaraka mbalimbali zinazohitajika kufikia Julai 15, 2018 kukamilisha na kuwasilisha HESLB ndani ya muda ulioongezwa,” alisema Badru katika taarifa yake

Alisema uhakika wa upatikanaji wa bahasha maalumu za kutuma maombi HESLB kwa mwaka 2018/2019 kuwa wanafanya kazi kwa karibu na Shirika la Posta Tanzania (TPC) na wamehakikishia kuwa wamesambaza bahasha za kutosha nchini kote ili kuwawezesha waombaji wa mikopo kutuma maombi yao kwa njia ya ‘EMS’ bila usumbufu.

“Kwa upande wa uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa vya waombaji wa mikopo na vile vya vifo vya wazazi wao, tumehakikishiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuwa maombi yote ya uhakiki wa vyeti yatakamilishwa ndani ya muda ulioongezwa.

“HESLB inawahakikishia waombaji wote wa mikopo kuwa maombi yao yatakayowasilishwa ndani ya muda uliotolewa yatapokelewa na kufanyiwa kazi,” alisema

Hata hivyo aliwataka waombaji wa mikopo kuusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2018/19’, ambapo mwongozo huo unapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.