Fifa yawaonya wapigapicha Urusi

Mtanzania - - Habari -

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), limewaonya wapiga picha na watangazaji nchini Urusi kwenye michuano ya Kombe la Dunia kutumia muda mwingi kuwaonesha wanawake warembo viwanjani wakati mchezo unaendelea.

Kiongozi wa shirikisho hilo, Federico Addiechi, ameweka wazi kuwa bodi ya soka kwenye michuano hiyo inapambana kupinga masuala ya kijinsia hasa kwenye Kombe la Dunia.

“Tayari tumeweza kupambana na watangazaji na wapiga picha mmoja mmoja hasa kwa wale ambao ni wenyeji hapa nchini Urusi. Kuna wakati wanaochukua picha za video wanahama kwenye soka na kuchukua picha za warembo huku mchezo ukiwa unaendelea.

“Hii inapigwa marufuku kwa kuwa picha hizo wanazivuta kwa kiasi kikubwa na kuwafanya watu wasahau kinachoendelea,” alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kwa kusema Fifa itawachukulia hatua wanahabari ambao watakuwa wanakiuka sheria hiyo kwa kipindi hiki kilichobaki.

Michuano hiyo inaendelea kesho huku Ubelgiji wakipambana na England kumtafuta mshindi wa tatu, kabla ya Jumapili kupigwa fainali kati ya Croatia dhidi ya Ufaransa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.