Wahanga reli ya kisasa kulipwa fidia

Mtanzania - - Habari - Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

ZAIDI ya wakazi 2,000 wa Dar es Salaam wamefanyiwa tathmini kulipwa fidia kupisha ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge).

Awamu ya kwanza ya ujenzi huo yenye umbali wa kilomita zaidi ya 400 kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma, inatarajiwa kukamilika mwaka 2019 na baadaye hadi nchi za Rwanda Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Masanja Kadogosa, alisema Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), ndicho kilipewa kazi ya kufanya tathmini hiyo na zaidi ya watu 2,000 wanatakiwa kupisha mradi huo.

“Tukishafanya tathmini kila mtu kabla hajalipwa anatakiwa asaini na asiporidhika tunafanya marekebisho, wale ‘valuer’ (wafanya tathmini) wanarudia,” alisema Kadogosa.

Aidha Kadogosa alizungumzia kuhusu madai ya fidia kidogo kwa wakazi wa Mtaa wa Gulukakwalala uliopo Kata ya Gongolamboto, Dar es Salaam.

Alisema kama kuna wananchi wana malalamiko ya fidia wayawasilishe kwao kwa sababu lengo ni kuhakikisha kila kinachofanyika Serikali haiibiwi na wananchi wanapata haki yao.

“Suala la fidia ni la kisheria kwa sababu unamfanyia mtu tathmini kulingana na bei ya soko, nia yetu mwananchi asipunjwe, lakini vilevile asiibie Serikali,” alisema.

Hivi karibuni, wakazi hao waliiomba Serikali kuangalia upya viwango vya fidia wanavyotakiwa kulipwa kulingana na eneo hilo.

Walisema wanakubali nyumba zao kubomolewa ili kupisha ujenzi wa reli hiyo, lakini hawakubaliani na fidia wanayotaka kulipwa.

Mmoja wa wakazi hao, Stephen Chivilime, alisema kutokana na viwango hivyo vya fidia, kwa hali ya sasa hawataweza kuwa na makazi kama ya awali na kuomba tathmini ifanyike upya.

“Tunaipenda reli na tunahitaji maendeleo kwa faida yetu, lakini kwa hali hii kuna hatari ya baba, mama na watoto kulala katika chumba kimoja. Tunaomba tathmini ifanyike upya na kama inawezekana tupatiwe na viwanja,” alisema Chivilime.

Mkazi mwingine, Monica Madata, alisema licha ya kumiliki nyumba ya vyumba vinne, anashangaa katika uthamini uliofanywa anatakiwa kulipwa fidia ya Sh milioni 1.1.

“Tunaomba Serikali iangalie upya fidia hizi ili haki itendeke, kwa sababu kwa fedha ninayotakiwa kulipwa Sh 1,188,000 hata kiwanja siwezi kununua,” alisema Monica.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.