Mradi wa kutunza mazingira waanzishwa Morogoro

Mtanzania - - Mkoa Tangazo - Na ASHURA KAZINJA

CHAMA cha Mazingira na Maendeleo kwa Umma Tanzania (CMMUT), kimeanzisha mradi wa kuhifadhi mazingira na bioanuwai ili kuinua hali ya maisha kwa wananchi katika misitu ya Uluguru.

Akizungumza wakati wa kukagua utekelezaji wa mradi huo shuleni unaofadhiliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF), Mwenyekiti Mtendaji wa CMMUT, Elibariki Kweka, aliyekuwa na kamati ya mipango miji na mazingira, alisema mradi huo umelenga kutoa elimu ya mazingira kwa wanafunzi shuleni.

Kweka alisema kwamba, kutokana na fedha nyingi kupelekwa kwa watu kwa ajili ya kupanda miti na kuhifadhi mazingira hasa ya Milima ya Uluguru bila mafanikio, chama hicho kimekuja na mbinu ya kuwapa elimu watoto shuleni na baadaye jamii kwa ujumla.

“Pesa nyingi zimetumika kuwapa watu kupanda miti na kuhifadhi mazingira, lakini tunaona bado uharibifu unaendelea.

“Kwa hiyo tumeamua tuwafundishe watoto wa shule na kuanzisha vilabu vya mazingira kwani tunaamini watoto wakianza kuelewa umuhimu wa mazingira wakiwa wadogo, watakapokuwa wakubwa watayatunza vizuri.

“Mradi huo unaohusisha upandaji miti ya matunda aina ya michungwa, miembe na miparachichi katika shule na tunaamini miti hiyo itawapatia wanafunzi chakula, kivuli na hata kuwainua kiuchumi kwa kuuza matunda hayo na kupata fedha zitakazowasaidia katika mahitaji mbalimbali,” alisema Kweka.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Boma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira, Amir Nondo, alitoa ushauri kwa walimu wa mazingira kuhakikisha wanafuata njia za kitaalamu katika kupanda na kuitunza miti hiyo vizuri ili iweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Bigwa, Lusato Musilanga, alisema mradi huo ni mzuri kwani unasaidia watoto kujifunza na kujua umuhimu wa kutunza mazingira.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.