Sababu za mzunguko mdogo wa fedha zatajwa

Mtanzania - - Habari Za Sabasaba -

MZUNGUKO mdogo wa fedha umechangia vikoba vilivyo chini ya Shirika la Equality for Growth (EFG), kupunguza kiwango cha fedha wanachokopeshana na riba kutoka Sh milioni saba hadi tano.

Akizungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa EFG, Shaaban Rulimbiye, alisema pamoja na vikoba hivyo kufikisha kiwango kikubwa cha fedha lakini marejesho yamezorota kutokana na hali ya uchumi masokoni.

Alisema baadhi ya vikoba mitaji yao imetetereka na hivyo kushindwa kurudisha fedha hizo kwa wakati.

“Mfano katika Soko la Kinyerezi jijini Dar es Salaam, walifikia kukopeshana hadi Sh milioni saba lakini sasa wamepunguza kutokana na wengi kushindwa kulipa kwa wakati,” alisema Rulimbiye.

Alisema hata hivyo wanachama wa vikoba hivyo wanakabiliwa na changamoto ya ubora wa bidhaa hivyo wanatafuta wafadhili wawezeshe utoaji elimu ya ufungashaji na vifungashio bora.

Alisema katika changamoto ya mitaji wamewakutanisha na taasisi za kifedha ambazo zipo tayari kuwaongezea mitaji kwa njia ya mikono.

“Wajasiriamali wetu tumewakutanisha na Baraza la Uwezeshaji Taifa ili waweze kupata fursa za mitaji na kusaidiwa kupata masoko nje ya nchi,” alisema Rulimbiye.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.