IOM yaipiga jeki Idara ya Uhamiaji

Mtanzania - - Kanda Ya Kaskazini - Na UPENDO MOSHA

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Wahamiaji (IOM), limekabidhi maabara yenye vifaa vya kisasa kwa Serikali ya Tanzania vitakavyotumika kuhakiki nyaraka mbalimbali zinazotumiwa na Idara ya Uhamiaji nchini.

Mwakilishi Mkazi wa IOM, Dk. Kassim Sufi, aliyasema hayo jana mjini Moshi, wakati wa makabidhiano ya maabara hiyo itakayokuwa ikichunguza pia pasi za kusafiria.

“IOM imekabidhi maabara iliyosheheni vifaa vya kisasa vya kuchunguza hati za kusafiria ili kubaini wale wote wanaoghushi nyaraka hizo pamoja na kudhibiti biashara haramu, ikiwamo ya binadamu

“Lengo la IOM ni kushirikiana na nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania, katika kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama wa raia inakuwa ni ya kutosha.

“Tumeamua kufanya hivyo kwa sababu changamoto zinazozikabili nchi mbalimbali barani Afrika ni pamoja na raia wa mabara mengine kuingia barani humu kwa kutumia nyaraka za kusafiria zilizoghushiwa na hivyo kutumia fursa hiyo kuingiza bidhaa za magendo.

“Yaani, watu mbalimbali ambao wamekuwa wakikamatwa kwa kujihusisha na biashara za magendo na kusafirisha watu kwa kutumia nyaraka feki kutoka Afrika kwenda Ulaya, wataanza kudhibitiwa kupitia maabara hii, kwani vifaa vilivyopo vina uwezo wa kutambua kwa haraka nyaraka feki,” alisema Sufi.

Kwa upande wake, Kamishina Jenerali wa Uhamiaji Nchini, Dk. Anna Makakala, alisema Serikali imejipanga vizuri kupambana na wahalifu wanaoghushi na kutumia vibaya hati za kusafiria za Tanzania.

Naye Mkuu wa Idara ya Utawala na Fedha, Makao Makuu ya Uhamiaji, Kamishina Edward Choghero, alisema kumekuwa na watu ambao wamekuwa wakichukua pasi za Tanzania na kuzitumia isivyo halali na kwamba idara hiyo itaendelea kuwadhibiti, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji cha Kikanda, Inocent Bazo, alisema maboresho ya vifaa hivyo yataboresha utoaji wa mafunzo na utendaji kazi kwa maofisa wa uhamiaji barani Afrika.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.