Wateja Tigo pesa kufurahia ubunifu mpya

Mtanzania - - Habari Za Biashara - Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WATUMIAJI wa huduma ya Tigo pesa sasa wanaweza kufurahia usalama zaidi kwa fedha zao hata pale inapotokea mteja amekosea namba na kutuma fedha kwa mtu asiyemkusudia.

Kupitia huduma mpya inayojulikana kama jihudumie, mteja anayekosea kutuma pesa anaweza kuzuia pesa hiyo kutolewa na kurudishiwa fedha zake kwa haraka.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mkuu wa Tigo anayeshughulikia huduma za kifedha kupitia mtandao, Hussein Sayed, alisema kupitia huduma hiyo mteja ataweza kujirudishia fedha zake endapo amekosea kuzituma pasipo kulazimika kupiga huduma kwa wateja.

“Kupitia huduma hii mteja hatahitaji kupiga huduma kwa wateja kuomba arudishiwe fedha alizotuma kwa bahati mbaya. Mara baada ya kugundua amekosea atatakiwa kufuata menyu ya huduma hii na ujumbe utatumwa kwa aliyetumiwa fedha kwa bahati mbaya na akiupokea na kuridhia fedha zirudi kwa mwenyewe atazipata ndani ya muda mfupi,” alisema.

Alisema huduma hiyo itapunguza uwezekano wa wanaotuma fedha na kukosea namba kupoteza fedha zao kwa kuwa inaweza kuzuia fedha kutolewa mara moja tofauti na kupiga huduma kwa wateja ambapo wakati mwingine atalazimika kusubiri kwa muda wakati wateja wengine wakihudumiwa jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa aliyetumiwa kuitoa fedha hiyo.

Pamoja na huduma hiyo, alisema kampuni ya Tigo inaendelea kuimarisha huduma yake ya Tigo pesa ili watumiaji wake waweze kuitumia kwa haraka na kwa urahisi katika kufanya shughuli zao zote zinazohitaji fedha.

“Tumeanza kampeni kubwa ya Tigo Pesa ni zaidi ya pesa ambapo pamoja na mambo mengine tunaendelea kuboresha huduma hii. Hivi karibuni tuliweza kuungana na Uber katika kuwarahisishia wateja wetu huduma salama ya usafiri na Masterpass QR kwa ajili ya kuwarahisishia huduma za manunuzi ya bidhaa na huduma,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.