Serikali yatakiwa kulipa deni wastaafu EAC

Mtanzania - - Habari Za Biashara - Na CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALÀAM

KAMATI ya Miundombinu imeitaka Serikali kulipa deni la Sh bilioni 4.99 la wafanyakazi wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambalo hivi sasa ni mzigo kwa Shirika la Posta nchini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso, amesema Serikali inalazimika kulipa kila mwezi kwa wastaafu hao 229 kiasi cha Sh milioni 74.

Kakoso alisema hayo katika ziara waliyoifanya katika shirika hilo na kueleza kuwa shirika hilo lilianza kupoteza mwelekeo hata baadhi ya watu walianza kulisahau hivyo Serikali inapaswa kushughulikia mara moja changamoto zinazojitokeza.

Alisema Serikali inapaswa ichukue mzigo wa madeni ya wafanyakazi hao na kama jambo hilo litafanywa kwa wakati litapunguza mzigo kwa shirika.

Mwenyekiti huyo alisema mpaka sasa shirika hilo limelipa zaidi ya Sh bilioni 5 na kwamba walikubaliana na Serikali kuwa watarejeshewa fedha hizo jambo ambalo halijafanyika mpaka sasa.

“Rasilimali zilizoko katika shirika la posta, halihitaji kupewa fedha na Serikali bali kuwezeshwa kwenye mifumo, kwani wao wana uwezo wa kujiendesha wenyewe,” alisema Kakoso.

Alisema shirika hilo Serikali ikiliwezesha linasimama lenyewe, lakini pia aliiomba Serikali isimamie deni la nyuma ambalo shirika hilo linadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) la Sh bilioni 26, ambalo limewekwa kwenye orodha ya mashirika yaliyofilisika.

“Jambo ambalo linaifanya Posta lisikopesheke mahali popote ni deni hilo, naomba mjitahidi kulipa,” alisema Kakoso. Alisisitiza kuwa mzigo wa madeni ya huko nyuma ambayo yanadaiwa kupitia TRA na fidia zake yashughulikiwe.

Aliongeza kuwa kama TRA watasimamisha faini na deni likabaki kama lilivyo, watalilipa kwa miaka 40 ndiyo liishe.

Aliiomba Serikali washughulikie hilo ili shirika libaki huru.

Kakoso pia aliiomba Serikali kuangalia mfumo wa kusaidia shirika la posta kwa washindani wake, ambao wao wamepewa masharti nafuu kuliko shirika hilo. Pia alishauri taasisi zote za Serikali kuanza kutumia huduma za posta, ili kufanya shirika hilo kuzalisha kwa viwango vikubwa.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alikiri kulipa pensheni ni jukumu la hazina na kwamba kuna mazungumzo yanaendelea serikalini jambo hilo litakaa vizuri.

Pia kwa upande wa deni la TRA, alisema kuna mazungumzo yanaendelea kuhakikisha Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Mapato Serikali (CAG), inafuta shirika hilo kutoka kwenye orodha ya waliofilisika.

Awali, Kaimu Meneja Rasilimali za Shirika la Posta, Morice Mbodo, alipokuwa akitoa mada kuhusu shirika hilo alikiri kuwa linalipa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Posta inaidai Serikali Sh bilioni 4.99.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.