Sanga apigwa chini Bodi ya Ligi

Mtanzania - - Habari Za Michezo - Na THERESIA GASPER - DAR ES SALAAM

KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemsimamisha Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Clement Sanga.

Sanga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, amekuwa akihudumu nafasi ya Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo tangu Yusuph Manji, ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa kupitia uchaguzi mkuu alipojiuzulu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema uamuzi wa kumwondoa Sanga katika nafasi hiyo unatokana na hatua ya Yanga kuwasilisha barua katika shirikisho hilo ukimtambulisha kama makamu mwenyekiti wa klabu hiyo na Manji ni mwenyekiti.

Alisema Kamati ya Utendaji ya TFF ilifikia uamuzi huo baada ya kikao chake kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana.

“Tulipata nakala ya barua ya Yanga kwenda kwa Manji kwamba Sanga si mwenyekiti, Manji ndiye mwenyekiti.

“Kulingana na katiba yetu, hana sifa tena ya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, uamuzi umezingatia mapendekezo ya Kamati ya Sheria, tayari tumemwandikia barua mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ili kuona namna ya kufanya, lakini pia kama kuna stahiki zake,” alisema Karia.

Katika hatua nyingine, Karia, alisema shirikisho hilo limeongeza idadi ya wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa na klabu za Ligi Kuu kutoka saba hadi kufikia 10.

“Tumeongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi 10, lakini tutakuwa wakali sana kuhakikisha vigezo vinazingatiwa katika kuwapata wachezaji,” alisema Karia.

Wakati huo huo, Karia alisema Kamati ya Utendaji ya TFF imemthibitisha rasmi, Wilfred Kidau, kuwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.