Mashabiki England washindwa kunywa bia

Mtanzania - - Michezo -

MASHABIKI wa timu ya taifa ya England, juzi walishindwa kumalizia bia baada ya timu hiyo kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi.

England wameondolewa kwenye michuano hiyo dhidi ya wapinzani wao Croatia kwa kufungwa mabao 2-1, katika mchezo wa nusu fainali.

England walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya tano lililofungwa na Kieran Trippier na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kumwaga bia na vinywaji mbalimbali kwa furaha huku wakiamini lingeweza kuwapeleka fainali, hatimaye mabao ya Ivan Perisic na Mario Mandzukic yaliweza kuzima ndoto za England kutinga fainali.

Perisic alisawazisha katika dakika ya 68 na kudumu hadi dakika 90, huku Mandzukic akifunga bao la ushindi ndani ya dakika 30 za nyongeza ambapo mashabiki wa England kila kona walipatwa na butwaa.

Idadi ya mashabiki jijini London ambao walikuwa wanafuatilia mchezo huo kwenye televisheni kubwa katika eneo la Hyde Park, walijikuta wakiondoka huku wakiacha bia mezani na wengine wakizimwaga kwa hasira.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa mashabiki wengine jijini Moscow walikuwa hawataki kupigwa picha na waandishi wa habari mara baada ya timu yao kuondolewa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.