Majaliwa aagiza eneo la Kiomoni lithaminiwe

Mtanzania - - Habari - Na MWANDISHI WETU -TANGA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema atamwagiza Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha kwenda katika Kata ya Kiomoni kufanya tathmini ya ardhi ya wananchi ili kubaini thamani halisi ya maeneo hayo waweze kufidiwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi hao kumlalamikia Waziri Mkuu kuhusu kutoridhishwa na fidia ya maeneo yao yaliyochukuliwa na Kampuni ya Neelkanth inayomiliki kiwanda cha kuzalisha chokaa.

Majaliwa alisema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kiomoni katika Mtaa wa Kiomoni wilayani hapa akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani hapa.

Alisema atamtuma Mthamini Mkuu aende kubaini nani anadai nini na anamiliki nini ili mwekezaji aweze kupewa kibali cha kuwalipa fidia yao.

“Tunataka jambo hili liishe, kabla ya mwishoni mwa mwaka huu kila kitu kiwe kimekamilika na hakuna mwananchi hata mmoja atakayepoteza haki yake ya msingi,” alisema Majaliwa.

Aliongeza kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwa kuwa ni sehemu ambayo viwanda mbalimbali vya saruji nchini vinategemea kwa kupata malighafi, hivyo alimpongeza mwekezaji na kumshauri aongeze uzalishaji kadiri anavyoweza. Alisema wawekezaji katika sekta ya viwanda ni muhimu kwa sababu wanaunga mkono mkakati wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ya kukuza uchumi kutoka wa chini hadi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda.

Majaliwa alisema fursa ya uwepo wa kiwanda hicho utawezesha kukuza uchumi wa taifa na wananchi kwa ujumla kwa sababu kiwanda kitakapokamilika kitatoa ajira ya watu zaidi ya 2,000 wakiwemo wakazi wa eneo hilo.

Wakati huo huo, Majaliwa alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa akutane na wananchi wa kijiji hicho na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.

Alisema Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili, na aliwataka viongozi wa wilaya hiyo kwenda kwa wananchi.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekani wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu hoja zote ni za ngazi ya halmashauri,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.