Idadi ya viumbe hai yazidi kupungua duniani

Mtanzania - - Jamii Na Afya - JOSEPH HIZA NA MTANDAO

IDADI ya viumbe hai na ikolojia duniani imeporomoka kwa kiwango cha kutisha kabisa katika kipindi cha miongo minne iliyopita. Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Mfuko wa Kimataifa wa Hifadhi wa Wanyamapori (WWF) iliyotolewa jana.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa idadi kubwa ya viumbe imepotea kutokana na uchu wa binadamu na shughuli zake, hali inayotishia ustawi wa siku za usoni.

Data za ripoti hiyo mpya iliyopewa jina la ‘sayari hai’ zinaonesha kuwa kwa ujumla idadi ya wanyama walio na uti wa mgongo inayojumuisha ndege, amfibia, reptilia, samaki na mamalia imepungua kwa asilimia 60 tangu mwaka 1970.

WWF imesema idadi ya viumbe vinavyoishi kwenye maji baridi hususani samaki, imeporomoka kwa wastani wa asilimia 83 kutokana na shughuli za ujenzi wa mabwawa makubwa, uvuvi uliopindukia, ongezeko la watu duniani pamoja na magonjwa yanayowakabili.

Ikolojia ya eneo la ukanda wa kitropiki la Amerika ya Kati na Kusini inakopatikana pia misitu ya Amazon ndiyo imeathirika zaidi kwa wastani wa asilimia 89, sababu kubwa ikiwa ni ukataji miti uliokithiri.

Kwa mujibu wa WWF, shughuli za kilimo na uwindaji wa wanyama uliokithiri, zimekuwa sababu ya kupotea kutoka uso wa dunia kwa hadi asilimia 75 ya viumbe kama mamalia, ndege, reptilia, amfibia na mimea.

Tishio jingine lililoangaziwa na ripoti hiyo ni suala la makazi ya viumbe, ambapo takwimu mpya zinaonesha ni robo pekee ya eneo la ardhi duniani lililobaki katika hali ya asili huku maeneo ya ardhi oevu yakipungua hadi asilimia 87 kutokana na watu kujenga juu ya maeneo hayo, ongezeko la watu na mabadiliko ya tabia nchi.

Ongezeko la joto linalotokana na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa pia limekuwa tishio kwenye ikolojia ya bahari ambapo nusu ya

matumbawe ambayo ndiyo chanzo cha uhai kwa hadi robo ya viumbe vya baharini imepotea.

Mwezi uliopita, jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilionya kuwa hata ikiwa dunia itafanikiwa kupunguza ongezeko la joto kwa kiwango cha nyuzi 1.5 bado itakuwa vigumu kuzuia kupotea kwa matumbawe.

WWF imeonesha pia wasiwasi wa kupotea kwa viumbe vinavyosaidia uchavushaji mimea ikiwamo nyuki, nondo, vipepeo, popo na jamii nyingine za ndege kutokana na matumizi makubwa ya dawa za kuua wadudu na kubadilishwa kwa matumizi ya ardhi kuwa miji.

Ripoti hiyo imetoa wito wa hatua za dharura kukabiliana na hali hiyo katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Ripoti hiyo inakuja huku ripoti nyingine tano zilizotolewa mapema

mwaka huu wakati wa Mkutano Mkuu wa Viumbe Hai wa Umoja wa Mataifa mjini Medellin, Colombia zikiwa zimetahadharisha juu ya hali mbaya ya viumbe hai duniani na kushauri namna ya kuikabili.

Wajumbe 750 kutoka nchi 115 walikutana katika kikao cha sita cha Jukwaa la Kisayansi na Sera Baina ya Serikali juu ya Viumbe Hai na Mfumo wa Ikolojia (IPBES).

Jukwaa hilo lilipewa kazi na Umoja wa Mataifa mwaka 2012 kutoa ushahidi bora zaidi ili kuweza kutoa uamuzi bora wa sera ya jinsi ya kulinda mazingira wakati ambapo dunia inaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa la mabadiliko ya tabia nchi.

Ripoti hizo tano, ambazo zilitayarishwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na wataalamu wa kimataifa wapatao 550, zinatoa tathmini ya kikanda juu ya mwenendo wa viumbe hai barani Afrika, Amerika Kaskazini na Amerika Kusini, Asia Pasifiki, Ulaya na Asia ya Kati. Ripoti ya tano inatoa tathmini juu ya hali ya uharibifu wa ardhi duniani kote.

Ripoti hizo zilihitimisha kuwa upande wa Amerika, spishi zimepungua kwa asilimia 31 ikilinganishwa na wakati walipowasili walowezi kutoka Ulaya. Athari za mabadiliko ya tabia nchi zikiwa zinaongezeka zimechangia sababu nyingine, kupotea huko kwa spishi kunatabiriwa kufika asilimia 40 ifikapo mwaka 2050.

Katika Afrika, kilomita 500,000 za mraba za ardhi tayari zinakadiriwa kuwa zimeharibiwa na matumizi makubwa ya rasilimali za asili, mmomonyoko wa ardhi, myeyusho wa chumvi na uchafuzi wa mazingira.

Katika Umoja wa Ulaya, ni asilimia saba pekee ya spishi za baharini na asilimia tisa ya aina za viumbe vinavyoishi baharini zinaonesha hali nzuri ya hifadhi. Asilimia 66 ya aina za viumbe vinavyoishi baharini inaonyesha hali mbaya ya hifadhi na aina nyingine zimeorodheshwa kama hazijulikani.

Kanda ya Asia-Pasifiki imeonyesha matokeo ya kutia moyo zaidi. Miaka 25 iliyopita, maeneo ya bahari yanayohifadhiwa katika kanda hiyo yameongezeka kwa takriban asilimia 14 na maeneo ya ardhini yanayohifadhiwa yameongezeka kwa asilimia 0.3. Maeneo ya misitu yameongezeka kwa asilimia 2.5.

Ripoti hizo pia zimegundua ukosefu wa maendeleo katika mipango mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kuhusu viumbe hai, ikiwa ni pamoja na Mpango Mkakati wa Viumbe Hai 2011-2020 na malengo yanayohusu viumbe hai, yaliyofikiwa na makundi tofauti wakati wa kusaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu viumbe hai huko Aichi, Japan mwaka 2010.

Pamoja na kuonesha hali ya kutisha, ripoti hizo pia zimetoa matumaini mapya ya kupambana na tatizo hilo.

Mapendekezo maalum yalitolewa kuhusu jinsi watunga sera wanavyoweza kusitisha au kurekebisha uharibifu wa viumbe hai katika maeneo tofauti.

“Zikiwekwa pamoja, ripoti hizi tano za ukaguzi zinawakilisha mchango muhimu wa kitaalamu kuhusu viumbe hai na mfumo wa ikolojia wa miaka 10 iliyopita,” anasema Robert Watson, Mwenyekiti wa mkutano huo.

Anasema: “Tathmini hizi zitatoa ufahamu ambao haukuwahi kushuhudiwa juu ya hali ya viumbe hai duniani na ubora wa ardhi, vitu viwili ambavyo ni muhimu kwa ubora wa maisha, afya na mifumo ya ikolojia.”

Uhitaji wa hatua haujawahi kuwa muhimu zaidi kuliko wakati huu tulionao.

Kati ya 1970 na 2012, uti wa mgongo wa hisa za kila mwaka zilipungua kwa zaidi ya nusu duniani kote.

Wakati huo huo, kila mwaka binadamu hutumia rasilimali nyingi zaidi kuliko uwezo wa dunia. Matokeo yake ni kwamba tunaharibu mifumo muhimu ya ekolojia.Madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yatasababisha tatizo kuwa baya zaidi, isipokuwa pale wasimamizi watakapochukua hatua.

Anne Larigauderie, Katibu Mtendaji wa IPBES, anaamini ushahidi mpya uliotolewa utahamasisha kuchukuliwa hatua.

“Kuna ufahamu mkubwa wa haja ya mazingira kujumuishwa katika mipango yote ya maendeleo na IPBES inajivunia kuwapa wanaotoa uamuzi duniani kote ushahidi wanaouhitaji ili kutunga sera na kuchukua hatua bora zaidi,”anasema.

Makala hii imeandikwa kwa msaada wa DW

Shughuli za binadamu zinatajwa kuwa tisho la viumbe hai

Viumbe vya baharini

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.