Serikali yapiga marufuku makubaliano wakulima, wafugaji

Mtanzania - - Kanda - Na SAFINA SARWATT

SERIKALI imepiga marufuku wafugaji na wakulima kuingia makubaliano ya kuingiza makundi ya mifugo kwenye mashamba ya wakulima. Agizo hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante ole Gabriel, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa kutatua migogoro ya wafugaji wa jamii ya Kimasai na wakulima wa vijiji vinane katika Kata ya Kia, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika maelezo yake, Profesa Ole Gabriel, alisema Serikali haipo tayari kuona wafugaji wanaonewa wala wakulima wakionewa.

“Wakulima hawana mipaka na kutokana na changamoto hizo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo ya kudumu kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.

“Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kutafuta suluhisho la kudumu la migogoro ya wafugaji wa jamii ya Wamasai pamoja na wakulima.

“Ieleweke kwamba, asilimia 98.7 ya wakulima katika nchi yetu ni wafugaji na hakuna haja kwa wakulima na wafugaji kugombana kwa kuwa wanafanya shughuli zinazotegemeana.

“Wafugaji hapa nchini wanapaswa kufahamu kwamba Serikali imeweka mikakati hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha wafugaji na wakulima wanapata maeneo ya kudumu.

Wakati huo huo, Profesa Ole Gabriel, alikemea tabia ya baadhi ya watumishi kugeuza mashamba ya ranchi za Taifa na Narco kuwa sehemu ya mitaji yao.

Alisema Serikali haitaruhusu vitendo vya rushwa katika mashamba ya Narco na ranchi za Taifa kwa kuwa maeneo hayo yanamilikiwa na Serikali. Akizungumzia mgogoro wa wananchi na Kampuni inayosimamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO), alisema atafanya mazungumzo na makatibu wenzake wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.