Banka kutoka kifungoni Februari

Mtanzania - - Michezo - Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kiungo, Mohammed Issa ‘Banka’, ataruhusiwa kuendelea kucheza soka ifikapo Februari 8 mwakani kwa kuwa atakuwa amemaliza adhabu ya kufungiwa kucheza soka kwa miezi 14.

Banka anatumikia adhabu hiyo baada ya Kamati ya Kuzuia na Kupambana na Dawa Zisizoruhusiwa Michezoni (Rado) Kanda ya Afrika, kumkuta na hatia ya kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Kiungo huyo ambaye msimu uliopita aliichezea Mtibwa Sugar kabla ya kusajiliwa na Yanga msimu huu, alibainika kutumia bangi baada ya kutiliwa shaka wakati akiichezea Zanzibar katika michuano ya Chalenji ya Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), iliyofanyika mwaka jana nchini Kenya.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, alisema adhabu dhidi ya mchezaji huyo ilianza kufanya kazi Desemba 9, mwaka jana, huku ikipangwa kumalizika Februari 8, mwakani.

Alisema baada ya kufanyiwa vipimo, kiungo huyo alikiri kutenda kosa.

“Alitakiwa kukubali au kukataa matokeo ya uchunguzi, lakini yeye alikiri kutumia, alitakiwa kutoa utetezi ambao aliamua kuwasilisha maandishi na alifanya hivyo Agosti mosi mwaka huu.

“Adhabu hiyo ingeweza kuwa kubwa zaidi na kufikia kufungiwa maisha, lakini kamati iliona umri wake ni mdogo, pia amejutia kitendo hicho na kuahidi kuwa balozi mzuri wa kupinga matumizi ya dawa hizo zisizoruhusiwa michezoni,” alisema Ndimbo.

Katika hatua nyingine, Ndimbo alisema TFF haitambui kama Banka ni mchezaji wa Yanga kwa kuwa shirikisho halikumwidhinisha kuichezea klabu hiyo ya Jangwani.

“Kutokana na sakata hilo, Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) liliamuru Banka asihamishwe hadi hatima ya sakata lake hilo litakapobainishwa,” alisema.

Lakini Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten, alipoulizwa kuhusu msimamo huo wa TFF alisisitiza kuwa Banka ni mchezaji wao halali kwa madai kwamba klabu yake ilikamilisha taratibu zote za usajili.

“Banka ni mchezaji wetu halali, tulifuata taratibu zote za usajili, kama unavyojua tumekuwa tukitumia mfumo wa usajili wa kisasa wa Fifa ambao walimthibitisha, lakini hakutumika kutokana na TFF kutotoa leseni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.