KMC yashtuka usingizini, yaibomoa Ndanda

Mtanzania - - Michezo - Na THERESIA GASPER -DAR ES SALAAM

TIMU ya KMC ya Kinondoni imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ushindi huo ni wa pili kwa KMC ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, baada ya kupanda daraja msimu uliopita.

Ushindi wa kwanza kwa timu hiyo inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ulikuwa wa mabao 2-0 dhidi ya Stand United, mchezo ambao pia ulirindima kwenye Uwanja wa Uhuru.

Baada ya matokeo ya jana, KMC ilifikisha pointi 13 na kukamata nafasi ya 13, baada ya kushuka dimbani mara 13, ikishinda mara mbili, sare saba na kuchapwa mara tatu.

Mabao ya KMC katika mchezo huo yalifungwa na Omari Ramadhani, dakika ya 13, huku mengine yakipachikwa na James Msuva, dakika za 59 na 79.

Kipindi cha kwanza kilitawaliwa zaidi na wenyeji ambao walifanya mashambulizi mengi, lakini hadi kipindi cha kwanza kinamalizika KMC ilikuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, KMC ilizidisha mashambulizi kwa lengo la kuongeza mabao zaidi na Ndanda kutaka kusawazisha, lakini mambo yalionekana kuwa mazuri kwa wenyeji ambao walifanikiwa kufunga mabao mengine mawili na kufanya dakika 90 zimalizike kwa wageni kuchapwa mabao 3-0.

Kichapo hicho kiliifanya Ndanda FC ikamate nafasi ya 15 katika msimamo, baada ya kujikusanyia pointi 12 sawa na Lipuli FC iliyoko nafasi ya 14 kutokana na tofauti ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.