Rais wa soka Ghana afungiwa maisha

Mtanzania - - Habari - ACCRA, GHANA

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), limetangaza kumfungia maisha aliyekuwa Rais wa zamani wa Chama cha Soka nchini Ghana (GFA), Kwesi Nyantakyi, kutokana na kashfa za rushwa.

Hata hivyo, mbali na kufungiwa maisha, lakini kiongozi huyo anatakiwa kulipa faini ya Swiss Franc 500,000 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 1 za Kitanzania.

Fifa imeweka wazi kuwa, Nyantakyi hatakiwi kujihusisha na masuala yoyote ya michezo kuanzia ngazi ya uongozi ndani ya taifa au kimataifa.

“Nyantakyi amefungiwa maisha kujihusisha na masuala ya michezo ndani ya nchi yake na kimataifa kutokana na kashfa ya rushwa pamoja na mambo mengine mengi kama vile kukiuka maadili ya shirikisho la soka la kimataifa.

“Kutokana na hali hiyo, Nyantakyi, atatakiwa kulipa faini ya CHF 500,000 kutokana na kitendo hicho, hiyo itakuwa onyo kwa viongozi wengine ambao wamekuwa wakitumia ofisi vibaya,” walisema Fifa.

Nyantakyi alichaguliwa kuwa rais wa chama hicho cha soka nchini Ghana mwaka 2005 na baadaye akaja kuwa mkuu wa umoja wa michezo wa Afrika Magharibi, akichukua nafasi ya Amos Adanu ambaye alikutwa na kashfa ya rushwa mwaka 2011.

Nyankakyi alianza kuchunguzwa na Fifa tangu Juni mwaka huu, hivyo ilifikia hatua ya kujitoa katika nafasi tatu tofauti ndani ya shirikisho hilo huku akiwa amepewa siku 90 za kusimamishwa wakati uchunguzi ukiendelea.

Juni mwaka huu chama hicho cha soka nchini Ghana, kilionekana kukutwa na kashfa mbalimbali mara baada ya Waziri wa Michezo, Kwame Asiamah, kutaka uchunguzi ufanyike. Agosti mwaka huu Fifa ilitangaza Kamati ya Normalization kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina ili kukifanya chama hicho kuwa imara.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.