Msichana Initiative yatoa elimu mimba za utotoni

Mtanzania - - Habari - Na RAMADHAN HASSAN -CHAMWINO

MSICHANA Initiative imezindua klabu 22 za Msichana Amani kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi wilayani hapa na Kongwa, lengo likiwa ni kuelimisha wanafunzi wa shule hizo kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni, kujiamini na kujitambua.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa klabu hizo katika shule ya Sekondari Mlowa Barabarani wilayani hapa jana, Ofisa Mawasiliano kutoka Msichana Initiative, Sara Beda alisema lengo la kuzianzisha ni kuelimisha wanafunzi juu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni, kujiamini na kujitambua.

Alisema kutakuwa na mada mbalimbali ambazo watajifunza wanafunzi hao ambazo ni afya, kujitambua, ukuaji, usawa wa kijinsia, mimba za utotoni, ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia, ukeketaji, kufahamu haki, utambuzi wa hisia na huruma.

“Awali tulijikita kwa wanawake tu ila kwa sasa ni kwa wote, ndiyo maana jina letu Msichana ni mwanamke na Amani ni mwanaume.

“Lengo letu ni kutoa elimu kuhusu madhara ya mimba za utotoni, ndoa za utotoni na kujiamini na kujitambua,” alisema Sara.

Ofisa Utawala wa Msichana Initiative na Mratibu wa Klabu Mashuleni, Lightness Njau alisema sababu ya kupeleka mradi huo Kongwa na Chamwino ni kutokana na wanafunzi wa kike wengi katika wilaya hizo kupewa mimba wakiwa shuleni.

Alisema kupitia klabu hizo wataweza kuwajengea uwezo na kuwafikia zaidi ya wanafunzi 5,000 wa shule za msingi na sekondari.

“Tunataka wanafunzi wafikie malengo yao, hivyo tutakuwa na klabu 22 ambazo 11 zitakuwa Kongwa na 11 zingine zitakuwa Chamwino,” alisema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mlowa Barabarani, Nandi Jofrey alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya wanafunzi kupewa mimba huku sababu akizitaja ni kushindwa kujitambua.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.