Junako kuajiri Watanzania 1,200

Mtanzania - - Mkoa - Na GUSTAPHU HAULE

KAMPUNI ya Kitanzania ya Junako inayojishughulisha na uingizaji wa madawa ya kutibu maji nchini, inatarajia kuajiri watu zaidi ya 1,200 baada ya kukamilisha ujenzi wa viwanda vyake viwili vinavyojengwa eneo la Misufini, Mlandizi, Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani pamoja na Mapinga Wilaya ya Bagamoyo, mkoani humo.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni hiyo, Comfort Kalugendo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na MTANZANIA kwenye maonyesho ya bidhaa za viwandani yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba, vilivyopo Picha ya Ndege, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Alisema kwamba, kiwanda cha kwanza ni kinachotengeneza dawa za kutibu maji kinachojengwa eneo la Misufini Mlandizi, Kibaha ambacho kitakamilika baada ya miezi 23 kwa gharama ya Sh bilioni 256.

“Kwa hiyo kukamilika kwa kiwanda hicho kutapunguza gharama za kuagiza dawa hizo kutoka nje na pia kitakuwa na uwezo wa kuuza nje bidhaa kwa asilimia 80 na asilimia 20 ya bidhaa hizo, zitakuwa zikiuzwa katika soko la ndani.

“Kwa sasa dawa hizo zinasambazwa nchini Uganda, Kenya, Dubai na Afrika Kusini. Kwa hiyo, kuwapo kwa kiwanda hicho kutasaidia kupanua wigo wa biashara katika soko la kimataifa.

“Pamoja na kiwanda hicho, kampuni imeanza mchakato wa kujenga kiwanda kingine cha kutengeneza mita za maji Wilaya ya Bagamoyo na kitakapokamilika, kitasaidia kuwarahisishia wananchi kulipa bili zao kulingana na matumizi.

“Kwa sasa mita tunazotengeneza ni zile ambazo mwananchi analipa baada ya kutumia, lakini mita mpya zitakazokuja mtumiaji atalipa kabla ya matumizi mtindo ambao utakuwa unafanana na Luku za umeme,” alisema Kalugendo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.