Manyanya ataka nguvu udhibiti bidhaa bandia

Mtanzania - - Habari - Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

NAIBU Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, amesema udhibiti wa bidhaa bandia ni sehemu muhimu ya uimarishaji wa biashara na uwekezaji nchini.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa, wakati akifungua mafunzo kwa Maofisa Upelelezi wa Mikoa na Wilaya wa Kanda ya Kati kuhusiana na udhibiti wa bidhaa bandia.

Alisema udhibiti wa bidhaa bandia ni sehemu muhimu ya uimarishaji wa biashara na uwekezaji nchini hivyo maofisa hao wa polisi wanatakiwa kuwa ni sehemu ya kuhakikisha wanasaidia kutokomeza bidhaa bandia.

Alisema uchumi jumuishi unategemea viwanda hivyo kama soko litakuwa limejaa bidhaa bandia azma ya Tanzania ya viwanda itashindwa kutimia.

“Serikali ya Awamu ya Tano haitaki kusikia habari ya bidhaa bandia hivyo kupitia mafunzo haya tunataka jambo hili liwe historia,” alisema.

Naibu Waziri huyo alisema wafanyabiashara wengi hawana elimu kuhusiana na bidhaa bandia hivyo FCC ina wajibu wa kuwapa elimu ili kudhibiti bidhaa hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), John Mduma, alisema FCC kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limeweza kutekeleza operesheni mbalimbali za kudhibiti uhalifu unaohusisha bidhaa bandia.

Alizitaja operesheni hizo kuwa ni pamoja na operesheni Mamba iliyoongozwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na za mikoani za udhibiti wa bidhaa bandia iliyoongozwa na Tume ya Ushindani (FCC).

“Hili ni jambo la kujivunia na mafunzo haya tutarajie makubwa kwani yatawaongezea maarifa maofisa wa Jeshi la Polisi katika kudhibiti bidhaa bandia,” alisema.

Alisema kwa kuwa uchunguzi wa makosa ya kijinai unaozalisha kesi huwa unaenda mahakamani na hufanywa na Jeshi la Polisi, hivyo Jeshi hilo lina jukumu kuchunguza na kuendesha mashtaka dhidi ya makosa yanayohusiana na bidhaa bandia.

“Hivyo basi kuwajengea uwezo Jeshi la Polisi ni suala la lazima na la muhimu katika kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.