Rais Trump apata pigo, Democratic wadhibiti Bunge

Mtanzania - - Leo Ndani - WASHINGTON, MAREKANI

CHAMA cha Democratic kimerejesha udhibiti wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha Rais Donald Trump, Republican baada ya kushinda wingi wa viti katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa Rais Trump kwa vile imeonesha si tu wapigakura wamemhukumu bali pia yatakwamisha sera zake.

Wakati matokeo ya viti zaidi ya 30 yakiwa bado kutolewa jana asubuhi, lakini yakielekea kuipa ushindi Democratic, chama hicho cha upinzani kilikuwa tayari kimejitwalia viti 221 dhidi ya 193 vya Republican.

Kwa kuwa na wingi wa viti, wana-Democratic watasimamia Kamati Kuu mbalimbali na kuwa na nguvu ya kutaka kupewa maelezo ya ulipaji kodi ya Rais Trump na kuchunguza uingiliaji wa Urusi wakati wa uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, ambao ulilenga kumsaidia kiongozi huyo katika kampeni zake.

Ushindi wa Democratic bungeni si jambo zuri kwa Rais Trump, na sasa atakabiliwa na upinzani maradufu katika kutekeleza sera zake kwa miaka miwili iliyobaki kwenye muhula wake wa uongozi.

Kiongozi wa Democratic, Nancy Pelosi ameutaja ushindi huo kuwa mwamko mpya wa Marekani.

Nancy alisema; “Bunge la Democratic litatafuta suluhu na kulileta taifa pamoja kwa sababu wote tumeshuhudia mgawanyiko nchini Marekani.

“Wamarekani wanataka amani. Wanataka matokeo. Wanataka sisi kufanya kazi ili kupata matokeo mazuri yatakayobadilisha maisha yao.”

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Habari la Associated Press, asilimia 25 ya wapigakura walitaja masuala ya afya na uhamiaji kuwa muhimu katika uchaguzi huo.

Kadhalika umeonesha kuwa wapigakura walimchukulia Trump kuwa sababu ya wao kupiga kura.

Lakini pia Rais Trump ameonekana kujigamba baada ya chama chake kusalia na viti vingi katika Baraza la Seneti, licha ya udhibiti wake katika Bunge hilo kuonekana kuyumba.

Wa-Repulican walikuwa na viti 51 katika baraza hilo dhidi ya 45 vya wa-Democratic, huku vikisalia viti vinne.

Kwa ujumla kulingana na utafiti wa uchaguzi huo, wapigakura sita miongoni mwa 10 walisema Marekani inaelekea pabaya, lakini wengine wakautaja uchumi wa nchi hiyo kuwa bora au mzuri.

Uchaguzi huu wa katikati ya muhula umeweka wazi usahihi wa wapigakura katika masuala ya kabila, jinsia na elimu, na huenda ukarekebisha sura ya siasa za Marekani katika miaka ijayo.

Kwa upande wa uchaguzi wa ugavana, Republican kufikia jana mchana walikuwa wamepoteza viti saba.

MATOKEO: Wafuasi wa Rais Donald Trump wakipozi wakati wakisubiri matokeo ya ugavana wa Florida jimboni humo jana. Mshirika wa rais huyo, Ron DeSantis alishinda kiti hicho dhidi ya Andrew Gillum wa Chama cha Democratic. – PICHA: PAP.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.