Madereva wa Serikali sasa kukamatwa

Mtanzania - - Habari - Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

MAKAMANDA wa polisi nchini wameagizwa kuwakamata na kuwaweka ndani madereva wa Serikali ambao wamekuwa wakivunja sheria barabarani.

Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF).

Katika swali lake, Sakaya alitaka kujua kuhusu madereva wa Serikali ambao wamekuwa wakivunja sheria za barabarani.

“Sheria inasemaje kuhusiana na madereva wa Serikali ambao wamekuwa wakivunja sheria au sheria zipo kwa watu wengine na sio madereva wa Serikali?” alihoji Sakaya.

Akijibu swali hilo, Masauni aliwaagiza makamanda wa polisi kuwakamata na kuwaweka ndani madereva wa Serikali ambao wamekuwa wakivunja sheria barabarani.

Aliwataka viongozi wa Serikali, wabunge na mawaziri kuhakikisha hawawi sehemu ya madereva wao kuvunja sheria za barabarani.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomari Khamis (CCM), alihoji kuhusu ajali zinazotokana na bodaboda na bajaji.

“Je, ni vijana wangapi wamepoteza maisha yao na wangapi wamepoteza viungo? Je, Serikali inatuambiaje sisi Watanzania kuhusiana na jambo hilo?” aliuliza mbunge huyo.

Akitoa majibu ya Serikali, Masauni alisema zaidi ya watu 800 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani huku zaidi ya 3,700 wakipoteza viungo.

Alisema tangu mwaka 2008 bodaboda na bajaji zilipoanza kutumika kama vyombo vya usafiri hadi kufikia Septemba mwaka huu, vyombo hivyo vimesababisha ajali 38,237.

“Watu waliopoteza maisha kutokana na ajali za bodaboda tangu mwaka 2008 mpaka Septemba mwaka huu ni 8,237 (sawa na watu 823 kila mwaka), waliopoteza viungo katika kipindi hicho ni 37,521 (sawa na watu 3,752 kila mwaka),” alisema Masauni.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.