Kuamka mapema kunapunguza uwezekano wa saratani ya matiti

Mtanzania - - Jamii Na Afya -

WANAWAKE wanaoamka mapema wana uwezekano mdogo wa kupata saratani ya matiti, kwa mujibu wa watafiti nchini Uingereza.

Hata hivyo, wanasayansi hao kutoka Chuo Kikuu cha Bristol nchini Uingereza wanakiri sababu ya uhusiano wa muda wa kuamka na hatari ya saratani bado kufahamika.

Kwa sababu hiyo kuna kazi ya kufanya kuipata sababu hiyo na kwamba ugunduzi huo ni muhimu kwa kuwa unamuathiri zaidi mwanamke.

Matokeo hayo, ambayo hayajapitiwa na watafiti wengine zaidi ya hao yaliwasilishwa kwenye Mkutano wa Saratani wa NCRI mjini Glasgow, Scotland.

Wanasayansi wanasema kila mtu ana kile kinachofahamika kama saa ya mwili ambayo inaonyesha jinsi mwili unavyofanya kwa saa 24.

Hii inajulikana kwa kitaalamu kama circadian rhythm, na inaathiri kila kitu kutoka muda tunaolala, hisia zetu na hata hatari yetu ya kupatwa na mshtuko wa moyo.

Lakini si kila saa ya mwili ya kila mtu inayoonyesha muda ulio sawa.Watu wa asubuhi au kwa jina la utani walilopewa na watafiti hao ‘vipozamataza; (larks) yaani ndege wadogo wa familia ya laudidae; huamka mapema, hufanya kazi mapema na huchoka mapema.

Kadhalika watu wa jioni au ‘bundi’ huwa na wakati mgumu kuamka mapema, huwa wa mazoea ya kuchelewa kulala.

Kwamba vipozamataza wana asilimia 40 hadi 48 ya chini ya kupata saratani kulingana na wenzao bundi.

Pia utafiti ulibaini hatari zaidi ya saratani kwa wanawake wanaolala zaidi ya muda unaopendekezwa na wataalamu wa saa saba hadi nane usiku – sawa na zaidi ya asilimia za ziada 20 kwa kila saa iliyocheleweshwa.

Watafii walitumia njia moja ya kuchambua data inayojulikana kama Mendelian randomization, wakichunguza DNA inayoonyesha ikiwa fulani ni watu wa asubuhi au wa jioni.

Utafiti huo ulihusisha karibu wanawake 400,000 nchini Uingereza, ambao taarifa zao za vinasaba zilirekodiwa katika Benki ya Bio ya Uingereza au kama sehemu utafiti wa ubia na Chama cha Saratani ya Matiti nchini humo.

Walionyesha kuwa watu walio na jenetiki za kurauka mapema asubuhi walikuwa na hatari ya chini ya kupatwa na saratani ya matiti kuliko wale walio na tabia za kutoamka asubuhi.

Karibu mwanamke mmoja kati ya saba hupata saratani ya matiti nchini Uingereza katika maisha

yake.

Lakini uchunguzi huu uliangazia kiasi kidogo cha maisha ya mwanamke. Na katika kipindi hicho ilibainika watu wawili katika ya 100 wasiorauka mapema walipata saratani ya matiti ikilinganishwa na mmoja kati ya watu 100 waliomka mapema.

Hata hivyo, umri na historia ya familia pia ni baadhi ya masuala yanayochangia mtu kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata saratani.

Dk. Rebecca Richmond ambaye aliongoza utafiti huo anasema bado ni mapema kuwapa ushauri wa moja kwa moja wanawake juu ya suala hilo.

“Bado tunahitaji kujua kwanini

mtu anayechelewa kuamka yupo kwenye hatari kuliko yule anayeamka asubuhi mapema. Inabidi tufumbue fumbo hilo kwanza kabla ya mengine,” alisema.

“Baadhi wanadhani kwamba kukosekana uwiano baina ya saa zetu za kijamii na saa za kimwili kunaweza kutuweka katika hatari ya maradhi.”

Kwamba bado kuna maswali mengi, ambayo hayajapata majibu juu ya uhusiano wa kuwahi au kuchelewa kuamka na uwezekano wa kupata saratani.

Sayansi kwa kawaida huwa haitoi majibu ya uhakika kwa asilimia 100, lakini utafiti huu tayari unaonekana kuwa na mashiko.

Shirika la Afya Duniani

(WHO) katika moja ya tafiti zao wameonesha kujinyima usingizi ama kuusumbua mwili kutoka usingizini mapema kuna uhusiano na hatari ya kupata saratani.

Dk. Richard Berks kutoka taasisi ya Saratani ya Titi Sasa, amesema: “Matokeo ya utafiti huu yanaongeza ushahidi uliokuwepo juu ya uhusiano wa usingizi na saratani ya matiti,”

Lakini pia alisema utafiti zaidi unahitajika ili kupata majibu ya baadhi ya maswali ambayo bado yanagonga vichwa vya wanasayansi. Matokeo hayo yanaongezwa katika tafiti nyingine zilizobaini uhusiano wa usingizi, ambao uliona viwango vya juu miongoni mwa wanawake wanaofanya kazi zamu za usiku au miongoni mwa wale wanaolala katika mazingira yenye mwanga.

Wanasayansi wanasema ukitaka kuishi hadi uzeeni na kuwa na afya nzuri ni lazima ulale masaa mengi iwezekanavyo na mazingira tulivu.

Magonjwa ambayo huua watu kwenye nchi zinazoendelea yana uhusiano fulani na kukosa kulala yakiwemo ya moyo. uzani wa mwili kupita kiasi, kisukari, msongo wa akili na kujiua.

Kwa mujibu ya wanasayansi, saa ambazo mtu anastahili kulala ili apate kuwa na afya nzuri ni kati ya saa saba na nane.

Unapolala chini ya saa saba, mwili wako unaanza kukumbwa na matatizo ya kiafya ikiwemo ukosefu wa kinga ya mwili.

Iwapo utashinda bila kulala kwa saa 20 mwili wako utakuwa katika hali sawa na mtu mlevi.

Moja ya tatizo la kukosa kulala ni kwamba hauwezi kugundua ni athari zipi zinazokupata.

Ni sawa na mlevi aliye kwenye baa, ambaye huchukua funguo za gari na kusema niko sawa.

Kila mfumo wa mwili wa binadamu hupata kujiunda upya wakati mtu analala na mfumo huu huathirika sana wakati mtu anakosa kulala.

Wanawake wanaoamka mapema wanapunguza uwezekano wa kupata saratani ya titi

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.