Benki ya NMB yamwaga misaada Korogwe, Kilindi

Mtanzania - - Biashara - Na MWANDISHI WETU -TANGA

BENKI ya NMB imetoa msaada wa madawati, vifaa vya afya, mabati, mbao na vifaa ya ujenzi kwa shule wilayani Korogwe na Kilindi mkoani Tanga, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 60.

Pamoja na vifaa hivyo vya kupaulia, pia NMB imekabidhi madawati 200 kwa ajili ya kupunguza uhaba wa madawati katika wilaya hizo.

Shule zilizofaidika na msaada huo kwa upande wa Korogwe ni Shule ya Msingi Mtonga iliyopata madawati 100, Shule ya Sekondari Semkiwa viti 50 na meza 50, Shule ya Msingi Kwasemangube mabati, kofia na misumari kwa Shule ya Msingi Kwamngumi, Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Shule ya Msingi Kijungumoto ya Halmashauri ya Mji Korogwe ambapo kila moja ilipewa msaada wa Sh milioni tano.

Kwa upande wa Wilaya ya Kilindi, Shule ya Sekondari Kimbe, imepata viti na meza 100, shule za msingi za Mafisa, Nkama na Songe zimepata mabati vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 20.

Pamoja na kutoa vifaa tiba kwa zahanati mbili kila moja Sh milioni tano na vifaa vyote kuwa na gharama ya Sh milioni 30.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa, aliishukuru Benki ya NMB kwa kutoa msaada wa madawati na vifaa vya ujenzi wilayani kwake na kusema msaada huo wa kijamii umewasaidia kukabiliana na changamoto za uhaba wa madawati na vifaa vya ujenzi wa madarasa kwenye sekta ya elimu.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhiwa madawati na mabati kutoka Benki ya NMB kwenye Shule ya Msingi Mtonga, Kasongwa, alisema pamoja na maendeleo makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwenye Sekta ya Elimu kwa elimu bila malipo, bado ni muhimu wadau kuchangia elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo, alisema vifaa tiba, madawati walivyopewa na Benki ya NMB vitasaidia kuboresha miundombinu ya shule na kuboresha afya za wananchi.

“Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, ipo kwenye maboresho makubwa ya huduma za jamii, lakini peke yake haitoshi mpaka kuwe na ushirikiano na wadau. Na leo hii NMB wamejidhihirisha kuwa ni wadau wetu wakubwa kwenye suala hili la huduma za jamii,” alisema Mtondoo.

– PICHA: IMANI NATHANIEL MKUTANO: Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini nchini (TAMIDA), Sammy Mollel, akizungumza katika mkutano wa wanachama Mkoa wa Dar es Salaam waliokutana jana kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazokikabili chama hicho. Kulia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dimitri Mantheakia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.