Skimu za umwagiliaji zapewa mikopo ya matreka Morogoro

Mtanzania - - Biashara - Na LILIAN JUSTICE -MVOMERO

WIZARA ya Kilimo kupitia Mfuko wa pembejeo wa Taifa (AGITF), umetoa mkopo wa matrekta yenye thamani ya Sh milioni 128 kwa vikundi vya skimu ya umwagiliaji za Kijiji cha Kigugu na Mbogo Kontonga wilayani Mvomero.

Hayo yalielezwa jana na mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo kupitia Mradi wa kuongeza tija na uzalishaji kwa zao la mpunga (ERPP), Henry Urio, wakati akizungumza kwenye sherehe za kukabidhi matrekra kwa skimu za umwagiliaji za Kigugu na Mbogo -Kontonga ambapo alisema zana hizo zitapelekea kuongeza zaidi uzalishaji.

Alisema kupatikana kwa zana za kilimo kulitokana na wakulima wa zao la mpunga katika vijiji hivyo kumwomba Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, ili kuwapatia zana hizo na hivyo kuachana na matumizi ya zana duni za kilimo.

“Mwaka jana wakulima hawa waliomba kusaidiwa zana hususan matrekta na ndio maana kupitia mfuko wa pembejeo wameweza kukopeshwa ili waweze kuzalisha kwa tija na kuachana na jembe la mkono,” alisema Urio.

Awali akikabidhi matrekta hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari, alisema katika Mkoa wa Morogoro kuna hekta milioni 1.5 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hivyo ni vyema wakulima wakachangamkia fursa hiyo zaidi na kujiongezea kipato chao. Kutokana na hali hiyo, aliwataka wakulima kuhakikisha mkopo huo wanaurejesha kwa wakati na kuumaliza ili mwisho wa siku waweze kuyamiliki wao wenyewe sambamba na kuwapa fursa pengine waweze kukopeshwa.

“Tunataka kuona matrekta hayo yanaongeza uzalishaji jambo ambalo litawezesha kilimo kufanyika kwa zaidi ya mara tatu kwa msimu, hivyo wakulima kuwa na uhakika wa kupata mavuno mengi,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.