Wakulima wa muhogo wapewa darasa

Mtanzania - - Biashara - Na CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM

WAKULIMA wa zao la muhogo nchini wametakiwa kuzingatia ubora wa zao hilo ili kuwezesha kupata soko la ndani na hata nje ya nchi.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana na mwekezaji wa zao hilo, Qiu Ruming, ambaye amesema ametembelea mikoa inayolima zao hilo na kushuhudia changamoto kwenye sekta nzima ya uzalishaji wa zao la muhogo.

Alisema katika ziara yake katika mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara, amebaini wakulima wengi uzalishaji wao si mkubwa hadi kulifanya zao la muhogo kuwa la biashara nje ya nchi.

“Wakulima wengi hawazingatii suala la ubora bali wingi wa uzalishaji kwenye mashamba yao hata namna bora ya uhifadhi wa mihogo kwa muda mrefu,” alisema Ruming.

Ruming alisema katika kuinua zao la muhogo nchini Tanzania, ipo haja ya kuweka mikakati ifuatayo kuwajengea uwezo wakulima wa zao hilo ili liwe la biashara.

Pia kufungua kiwanda cha kwanza kikubwa cha kuchakata mihogo wilayani Handeni mkoani Tanga na kufungua matawi ya viwanda vidogo kwenye wilaya zinazolima zao hilo.

Alisema pia ni vyema kutoa ushauri kwa wakulima na wadau wote wa namna zao hilo linaweza kuwa la biashara.

Alisisitiza kuwa mbegu bora ya mhogo katika kuongezea thamani kupitia wanga unaweza kutengeneza bidhaa za ujenzi kama ‘gypsum board’, makasha, madaftari, mafuta ya muhogo.

Alisema Tanzania ni nchi yenye fursa kubwa ya uwekezaji na anatarajia kurudi Desemba pamoja na watendaji wengine ili na wao waweze kubaini fursa zilizopo katika zao hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, alimshukuru mwekezaji huyo kwa kuja kujionea uzalishaji.

“Nashukuru Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kumleta mwekezaji wa zao hilo kwani Watanzania wengi wanazalisha zao la muhogo ila hawajui soko linahitaji nini,” alisema Gondwe.

Alisema mwekezaji huyo amekuja wakati mwafaka wa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, katika juhudi za kujenga uchumi wa viwanda.

Alisema watatatua changamoto tajwa ili kuboresha zao hilo liwe la kisasa na la kibiashara.

Aliongeza kuwa Wilaya ya Handeni imeweka mfumo mzuri kwa wakulima ya namna ya uzalishaji wa zao hilo.

Alisema kwa misimu miwili Wilaya ya Handeni, imeweza kulima ekari 190 na limeweza kuhudumia soko la ndani.

Gondwe alisema wanatarajia kuzalisha tani milioni 1.4 kwa mwaka huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.