Sita wakamatwa kwa kupanga kumshambulia rais Ufaransa

Mtanzania - - Kimataifa - PARIS, UFARANSA

MAOFISA wa Usalama nchini Ufaransa wamesema wamewakamata watu sita wanaoshukiwa kupanga njama za kumshambulia Rais Emmanuel Macron.

Ofisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema maofisa wa ujasusi wanawashikilia washukiwa hao sita katika maeneo matatu tofauti, mmoja akiwa maeneo ya milima ya Alps.

“Mpango huo wa kumlenga Rais wa Ufaransa ulionekana kutokuwa dhahiri na usiokamilika, lakini ulikuwa ni wa vurugu,” alisema ofisa huyo.

Serikali ya Ufaransa imesema washukiwa waliokamatwa, akiwamo mwanamke mmoja wana umri wa miaka kati ya 22 na 62.

Akizungumza na waandishi habari, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Christophe Castaner alisema washukiwa hao wanaaminika kuwa wanaharakati wanaoegemea siasa kali za mrengo wa kulia.

“Bila shaka nafahamu juu ya tukio hili, siwezi kulipuuza. Lakini bila shaka linahusiana na mtandao unaofungamana na siasa kali za mrengo wa kulia, ambao kwa muda sasa umekuwa ukipata nguvu na kuzusha vurugu.

“Uchunguzi uko wazi na kuanzia sasa utaendeshwa na mahakama,” alisema Waziri Castaner.

Marais wa Ufaransa wamekuwa wakilengwa mara kwa mara katika miongo kadhaa iliyopita.

Mwaka 2002 mwanachama wa mrengo huo wa kulia alijaribu kumshambulia Rais wa wakati huo, Jacques Chirac katika mtaa mashuhuri wa Champs-Elysees jijini Paris wakati wa sherehe za kitaifa za Bastille.

Hayo yalijiri wakati Rais Macron akiwa katika mji mmoja Kaskazini Mashariki wa Verdun jana, akihudhuria sherehe za kuadhimisha kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia.

Mpango huo wa kumshambulia Rais huyo wa Ufaransa, uligundulika siku kadhaa kabla Rais wa Marekani, Donald Trump na viongozi wengine wa dunia kuwasili hapa mwishoni mwa wiki iliyopita kuadhimisha miaka 100 ya kumalizika kwa vita hiyo ya kwanza ya dunia hapo Novemba 11.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.