Manula ahakikishiwa ufalme Simba

Mtanzania - - Mbele - Na THERESIA GASPER -DAR ES SALAAM

KIWANGO cha mlinda mlango wa Simba, Aishi Manula, kimemkosha kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, ambaye amefunguka kuwa atafanya usajili kwenye nafasi za ndani pekee kipindi cha usajili wa dirisha dogo.

Usajili wa dirisha dogo kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara litafunguliwa Novemba 15 na kuhitimishwa Desemba 15.

Manula ambaye amewahi kutwaa tuzo ya kipa bora kwa misimu miwili mfululizo, 2015-2016, 2016-2017 akiwa na kikosi cha Azam na 2017/18 akiwa na Simba, hadi sasa amecheza michezo 11 na kuruhusu mabao manne.

Mlinda mlango huyo namba moja wa timu ya Taifa, pia ameisaidia klabu yake ya Simba kucheza mechi tatu mfululizo bila kuruhusu bao katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons (10), Mbeya City (2-0) na Ndanda FC ambayo iliisha kwa suluhu.

Mbali ya Manula, Simba ina makipa wangine watatu ambao ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Ally Salim na Said Mohamed ‘Nduda’.

Akizungumza jana mara baada ya mazoezi ya kikosi cha Simba yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam, Aussems, alisema hatafanya usajili wa wachezaji wengi katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo, ila ataongeza nguvu katika maeneo machache.

“Nitasajili maeneo mengine kama ni mshambuliaji, kiungo au beki, lakini siwezi kugusa nafasi ya kipa kwa sababu waliopo wapo vizuri.

“Hutakiwi kusajili tu lazima ufanye hivyo kwa kuangalia mahitaji ya timu,” alisema.

Akizungumzia programu yao ya mazoezi katika kipindi hiki cha mapumziko kupisha michezo ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Aussems, alisema atatumia muda huo kucheza mechi za kirafiki.

“Kama mambo yatakwenda vizuri, tutacheza mchezo mmoja wa kirafiki na timu moja ya Ligi Daraja la Pili na nyingine moja ya kimataifa.

“Hatuna muda wa kupoteza kwa sababu tunataka kuwatumia zaidi wale wachezaji waliokuwa hawapati nafasi ya kutosha ya kucheza katika mechi zilizopita ili wawe fiti zaidi.

“Nadhani huu ni muda mwafaka wa wao kujiweka fiti zaidi ili watakapopata nafasi katika michezo ya ligi waweze kufanya vizuri,” alisema.

Simba inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imejikusanyia pointi 26 sawa na Yanga iliyoko nafasi ya tatu kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Manula ambaye amewahi kutwaa tuzo ya kipa bora kwa misimu miwili mfululizo, 2015-2016, 2016-2017

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.