Watozwa faini ya milioni 9/kwa tathmini ya mazingira

Mtanzania - - Leo Ndani - NA KULWA MZEE DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewatia hatiani wafanyakazi watatu wa Kampuni ya Jiangxi International (T) Investment Limited kwa kujenga bila kuchukua tathmini ya uharibifu wa mazingira.

Waliotiwa hatiani jana ni raia wawili wa China, Xia Yanan na Chen Jinchuan na Mtala Habibu ambao mahakama iliwahukumu kulipa faini ya Sh milioni 9.3 ama kwenda jela miaka 12 baada ya kukiri makosa mawili ikiwamo kushindwa kuchukua tathmini ya uharibifu wa mazingira.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya washtakiwa kukiri kutenda makosa hayo.

“Kwa kuwa washtakiwa wamekiri makosa yao bila kuisumbua mahakama, mahakama inawatia hatiani kwa makosa yote mawili.

“Mahakama yangu inawatia hatiani kwa makosa mawili, kila mshtakiwa atalipa Sh milioni tatu kwa kosa la kwanza au kwenda jela miaka miwili.

“Shtaka la pili, kila mshtakiwa atalipa Sh 100,000 au kwenda jela miaka miwili, kwa asiyeridhika haki ya kukata rufani iko wazi,” alisema Hakimu Shaidi.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na jopo la Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga, Patrick Mwita na Wakili wa Serikali Faraji Nguka uliwasomewa washtakiwa mashtaka yao.

Katuga akisoma mashtaka alidai kati ya Januari na Agosti 28, mwaka huu wilayani Kinondoni, washtakiwa wakiwa wajenzi wa mradi wa ujenzi uliopo Rejent Estate, waliendeleza ujenzi bila kuchukua tathimini ya uharibifu wa mazingira.

Alidai shtaka la pili, washtakiwa wanatuhumiwa kutokutii amri halali iliyotolewa Agosti 28, mwaka huu na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) ya kuwataka kusimamisha ujenzi wa mradi huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.