Same Kaya Saccos waanza kujipanga

Mtanzania - - Kanda - Na UPENDO MOSHA

CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo kiitwacho Same Kaya Saccos, kilichoko wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, kimepitisha mpango mkakati wa miaka mitano unaolenga kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kukuza mtaji wake.

Hayo yalibainishwa na Meneja wa Chama hicho ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi, Elvera Mdee, wakati akizungumza katika mkutano wao mkuu wa 16 uliofanyika jana wilayani humo.

Alisema kwamba, mpango mkakati wa chama hicho utakaotekelezwa kati ya mwaka 2018 hadi mwaka 2022, ukilenga kuwanufaisha moja kwa moja wanachama wake, pia umelenga kuboresha huduma za chama hicho ili kuleta tija na ufanisi katika kukuza uchumi.

“Mpango mkakati huu umelenga pamoja na mambo mengine, kuongeza thamani ya mikopo inayotolewa na chama chetu kutoka shilingi bilioni 1.2 za sasa hadi shilingi bilioni 2.1 ifikapo mwaka 2022.

“Pia, tumelenga kuongeza thamani ya mtaji wa chama kutoka shilingi milioni 283.9 za sasa na kufikia shilingi milioni 469, ifikapo mwaka 2022.

“Pia, mpango huo utakwenda sambamba na kuongeza idadi ya wanachama kutoka wanachama zaidi ya 4,000 walioko sasa hadi kufikia wanachama 5,110 ifikapo mwaka 2022. “Yaani pamoja na kujiwekea malengo mbalimbali, pia tunatarajia kuongeza bidhaa mpya sita za huduma katika kipindi hicho kwa ajili ya wanachama wetu na wateja wengine wa chama chetu ili kupata mapato mengi zaidi,” alisema. Mwenyekiti wa Ushirika huo, Elibariki Kisimbo, alisema chama hicho kimepiga hatua kimaendeleo baada ya kulipa madeni yake yote.

Naye mgeni rasmi katika mkutano huo, Samuel Nyiru, alitoa rai kwa uongozi wa Serikali wilayani humo, kushirikiana na ofisi ya idara ya ushirika ili kukabiliana na changamoto ya madeni ambayo alisema yanarudisha nyuma maendeleo ya chama hicho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.